2013-12-17 08:25:46

Happy Birth Day Papa Francisko kwa kutimiza Miaka 77 ya kuzaliwa kwako!


Baba Mtakatifu Francisko, tarehe 17 Desemba 2013 anaadhimisha Miaka 77 tangu alipozaliwa. Itakumbukwa kwamba, Kardinali Jorge Mario Bergoglio alichaguliwa kuwa Khalifa wa Mtakatifu Petro hapo tarehe 13 Machi 2013. Ni Papa wa 266 kuliongoza Kanisa Katoliki tangu enzi ya Mtakatifu Petro.

Baba Mtakatifu Francisko kadiri ya mapokeo na mtindo wake wa maisha ambao unaendelea kuwashangaza wengi, siku yake ya kuzaliwa hupenda kuiadhimisha akiwa amezungukwa na watoto, ili kumshukuru Mungu kwa Injili ya Uhai, tayari kusonga mbele kwa imani na matumaini kutangaza Injili ya Furaha kwa Watu wa Mataifa.

Mwishoni mwa Juma, Baba Mtakatifu alifanya kumbu kumbu ya kuzaliwa kwake kwa kutembelea Zahanati ya Watoto wadogo ya Mtakatifu Martha iliyoko mjini Vatican. Ilikuwa ni siku kuu ya kawaida iliyosheheni furaha inayobubujika kutoka katika maisha ya kifamilia. Baba Mtakatifu Francisko anaendelea kupokea salam na matashi mema kutoka sehemu mbali mbali za dunia, lakini kubwa zaidi anawaomba waamini na watu wenye mapenzi mema kuendelea kumwombea katika maisha na utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican inamtakia kheri na baraka katika maisha na utume wake kwa ajili ya Kanisa na Ulimwengu kwa ujumla, Mungu na mwanadamu wakipewa kipaumbele cha kwanza katika hali ya unyenyekevu na ujasiri mkuu.







All the contents on this site are copyrighted ©.