2013-12-16 08:13:18

Majembe mapya ya uongozi Umoja wa Watanzania wanaosoma Roma


Umoja wa wanafunzi wakatoliki watanzania wanaosoma mjini Roma, Jumapili iliyopita, tarehe 15 Desemba 2013 wamechagua viongozi wapya, watakaooongoza Umoja huu kwa kipindi cha Mwaka 2013- 2014. Uchaguzi huu umesimamiwa na Padre Dietrich Pendawazima, Makamu mkuu wa Shirika la Waconsolata pamoja na Dr. James A. Msekela, Balozi wa Tanzania nchini Italia na Mwakilishi wa Tanzania kwenye Mashirika ya Umoja wa Mataifa yenye makao yake mjini Roma. RealAudioMP3

Waliochaguliwa ni Padre Gaston Mkude kutoka Jimbo kuu la Dar es Salaam kuwa Mwenyekiti mpya. Wengine ni Shemasi Romanus Wissa aliyechaguliwa kuwa Katibu. Sr. Regina Siyumbu amechaguliwa kuwa mweka hazina; Padre Pambo Martini Mkorwe, OSB amechaguliwa kuwa kiongozi wa Ibada na Padre Clement Kihiyo amechaguliwa kuwa ni Mkutubi mkuu wa Nyaraka za watanzania wanaosoma Roma.

Balozi Msekela amewashukuru na kuwapongeza viongozi waliomaliza muda wao kwa kazi kubwa waliyoifanya katika kuwahudumia watanzania wenzao. Ni matumaini yake kwamba, viongozi wapya wataendeleza na kuboresha huduma hii makini kwa ajili ya mafao, ustawi na maendeleo ya watanzania na Kanisa katika ujumla wake.








All the contents on this site are copyrighted ©.