Mabalozi wa Vatican ni vyombo vya amani na upatanisho
Kwa mara ya kwanza Askofu mkuu Pietro Parolin, tangu alipoteuliwa na Baba Mtakatifu
Francisko kuwa ni Katibu mkuu wa Vatican, Jumamosi tarehe 14 Desemba 2013 amemweka
wakfu Monsinyo Aldo Giordano kuwa Askofu mkuu na Balozi wa Vatican nchini Venezuela,
mahali ambako Askofu mkuu Parolin alitekeleza utume wake kama Balozi wa Vatican hadi
kufikia Mwezi Septemba 2013. Ibada hii imefanyika Jimboni Cuneo, Kaskazini mwa Italia.
Askofu
mkuu Parolin ametoa salam na matashi mema kutoka kwa Baba Mtakatifu Francisko, anaendelea
kulihimiza Kanisa kutangaza Injili ya Furaha. Balozi na wawakilishi wa Khalifa wa
Mtakatifu Petro wanapaswa kutolea ushuhuda wa ujumbe huu kwa maneno na matendo yao
kati ya wakuu wa nchi na Jumuiya za Kikristo wanazozihudumia, ili kujenga na kuimarisha
umoja na mshikamano wa dhati.
Kama wawakilishi wa Vatican, wanapaswa kusaidia
mchakato wa ujenzi wa Kanisa mahalia, kuendelea kuwa ni kiungo makini kati ya Kanisa
la Kiulimwengu na Maaskofu mahalia; kwa njia ya utume huu wanajenga na kuimarisha
mshikamano na umoja wa Kanisa zima. Ni utume unaohitaji majitoleo na utayari wa kuishi
na kukutana na watu kutoka katika tamaduni, hali za maisha kijamii na kikanisa.
Askofu
mkuu Giordano kuanzia mwaka 1995 alianza kutekeleza utume wake wa kidiplomasia, kumbe
ni kiongozi aliyebobea katika maisha haya na kwamba, changamoto iliyoko mbele yake
ni kuendeleza mang’amuzi aliyojipatia katika masuala ya utume Barani Ulaya, ili kukabiliana
na changamoto za Uinjilishaji Mpya Amerika ya Kusini na kwa namna ya pekee kabisa
nchini Venezuela.
Askofu mkuu Parolin anasema, huko atakumbana na changamoto
za utandawazi, umaskini, ukosefu wa haki jamii, utengano kati ya Kanisa na masuala
ya kisiasa; maana ya upendeleo kwa ajili ya watu maskini, umuhimu wa vyombo vya mawasiliano
ya jamii na harakati za jamii inayotaka kumng’oa Mwenyezi Mungu katika vipaumbele
vya maisha yao. Hizi ni changamoto zilizofafanuliwa na Baba Mtakatifu Benedikto wa
XVI wakati wa ufunguzi wa mkutano wa Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Amerika
ya Kusini na Visiwa vya Carraibi huko Aparecida.
Nchini Venezuela changamoto
kubwa ni kuendeleza mchakato waupatanisho, haki na amani; ili kujenga na kudumisha
majadiliano na utashi wa watu kukutana pamoja ili kushirikishana tone la matumaini.
Askofu mkuu Giordano anaweza kutekeleza vyema utume wake nchini Venezuela kwa kutumia
mang’amuzi na uzoefu wa shughuli za kidiplomasia, lakini zaidi aongozwe na mwanga
wa Neno la Mungu.
Ibada hii ya Misa takatifu imehudhuriwa na Makardinali 6,
Maaskofu 30, wanasiasa na wanadiplomasia kutoka ndani na nje ya Jumuiya ya Ulaya,
30 pamoja na Mameya wa Manispaa kumi na nane.