2013-12-16 11:34:35

Mabalozi na wawakilishi wa Nchi na Mashirika ya Kimataifa wakutana na Katibu mkuu wa Vatican


Askofu mkuu Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican, hivi karibuni alikutana na kuzungumza na Mabalozi pamoja na wawakilishi wa Mashirika ya Kimataifa mjini Vatican, kama sehemu ya utambulisho wake kama katibu mkuu mpya wa Vatican. Alitumia fursa hii kuwatakia kheri na baraka kwa Siku kuu ya Noeli na Mwaka Mpya 2014.

Askofu mkuu Parolin katika hotuba yake kwa Mabalozi na wawakilishi hao, amewahakikishia kwamba, atakuwa nao bega kwa bega katika mchakato wa kutafuta haki, amani, utu na heshima ya binadamu wote, kwa kutambua kwamba, amani ambayo ni zawadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu inaweza kupatikana ikiwa kama kila mtu atatekeleza wajibu na dhamana yake ndani ya Jamii husika.

Kuna haja kwa Jumuiya ya Kimataifa kushirikiana kwa pamoja ili kujenga na kudumisha utamaduni wa amani, kwa kujibu kwa ujasiri changamoto zinazojitokeza ili kujenga na kuimarisha umoja na udugu katika Jumuiya ya Kimataifa. Baba Mtakatifu Francisko anaendelea kuwahimiza waamini kuwa ni vyombo vinavyotaka Injili ya Furaha inayopatikana katika uhalisia wa maisha ya mwanadamu.

Furaha ijikite katika misingi ya amani na uelewano kati ya watu; iwe ni msingi unaowawezesha watu kukutana na kubadilishana mawazo; kujadiliana na kujipatanisha! Huu ndio ubinadamu ambao Kanisa kwa kushirikiana na Jumuiya ya Kimataifa inapenda kujenga na kudumisha kati ya Watu wa Mataifa, ili kweli iweze kuwa ni Familia ya binadamu inayojikita katika majadiliano badala ya vita na kinzani; familia yenye nguvu inayojitaabisha kuwahudumia wanyonge.

Askofu mkuu Parolin anaendelea kubainisha kwamba, binadamu yuko katika hija ya kutafuta amani na matumaini ya leo na kesho iliyo bora zaidi. Baba Mtakatifu Francisko anawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema kuzima kiu hii na Kanisa kuendelea kutangaza, kushuhudia na kuwaonjesha watu Injili ya Furaha. Kanisa halina budi kuacha milango yake wazi kama kielelezo cha mwanga, urafiki, furaha, uhuru na hali ya kuaminiana.

Baba Mtakatifu anaendelea kulihamasisha Kanisa kuimarisha utamaduni wa kukutana na kushirikishana Injili ya Furaha inayobubujika kutoka kwa Kristo na Kanisa lake. Kipindi cha Majilio ni maandalizi ya Ujio wa Yesu Kristo, Masiha na Mkombozi wa dunia.







All the contents on this site are copyrighted ©.