2013-12-16 14:21:54

Kanisa linahitaji kuwa na roho ya Kinabii ili kuwatangazia watu Habari Njema!


Mama Kanisa anatumwa kutolea ushuhuda wa kinabii unaojikita katika Neno la Mungu na maisha ya kimungu yaliyomo ndani mwake. Nabii hana budi kusikiliza Neno la Mungu kwa umakini mkubwa, tayari kutangaza Ujumbe wa Mungu kwa wakati muafaka.

Ni mtu ambaye anatambua wakati uliopita, wakati uliopo na wakati ujao! Manabii katika Agano la Kale wamekuwa ni viongozi wakuu wa Taifa la Mungu, hasa nyakazi zile, walipokuwa wanatembea katika giza na hali ya kukata tamaa; nyakati ambazo Waisraeli hawakuwa na Hekalu, Yerusalemu ilipokuwa imevamiwa na watu kuanza kujiuliza ikiwa kweli Mwenyezi Mungu ni mwaminifu katika ahadi zake.

Ni sehemu ya mahubiri yaliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko, tarehe 16 Desemba 2013 Jumatatu ya tatu ya Kipindi cha Majilio, kwenye Kikanisa cha Mtakatifu Martha, kilichoko mjini Vatican. Baba Mtakatifu anasema, hii ndiyo hali aliyokumbana nayo Bikira Maria chini ya Msalaba. Manabii waliuwawa kwa sababu watu hawakupenda kusikia, kukumbatia na kumwilisha ahadi za Mungu katika maisha yao.

Ni watu ambao hawakusikia na wala kusoma alama za nyakati; wakamezwa na madaraka! Manabii ni watu wanaoamsha dhamiri za watu ili kusikia kwa mara nyingine tena Neno la Mungu na ahadi zake, utume na dhamana inayotekelezwa na Nabii.

Baba Mtakatifu anawaalika waamini wakati huu wanapoendelea kujiandaa kwa ajili ya kuadhimisha Fumbo la Umwilisho, kuombea kipaji cha unabii, kwa kutambua kwamba, kila Mkristo kwa njia ya Sakramenti ya Ubatizo ni Nabii, kwani anatumwa kutangaza Habari Njema ya Wokovu. Kanisa linahitaji kuwa na roho ya kinabii!







All the contents on this site are copyrighted ©.