2013-12-14 08:43:45

Udugu ni silaha dhidi ya umaskini, rushwa na ufisadi; udugu unalinda na kutunza mazingira


Udugu ni msingi na njia ya amani; ndiyo kauli mbiu inayoongoza Maadhimisho ya Siku ya 47 ya Kuombea Amani Duniani, itakayofanyika tarehe Mosi, Januari 2014 sanjari na Maadhimisho ya Siku kuu ya Bikira Maria Mama wa Mungu. Huu ni ujumbe unaochota utajiri wake kutoka katika Maandiko Matakatifu pamoja na mang'amuzi ya mshikamano wa kidugu kati ya watu.

Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwa ajili ya kuombea amani duniani anakazia mambo makuu yafuatayo: udugu kama msingi na njia ya amani; udugu kama nyenzo msingi katika mapambano dhidi ya baa la umaskini; kugundua tena umuhimu wa mshikamano wa kidugu katika masuala ya kiuchumi; udugu unaozima chokochoko za vita na kinzani za kijamii; udugu unaong'oa mizizi ya rushwa na ufisadi; udugu unaolinda na kutunza mazingira.

Huu ni ufafanuzi uliotolewa na Kardinali Peter Turkson, Rais wa Baraza la Kipapa la haki na amani na kusoma kwa niaba yake na Padre Federico Lombardi, msemaji mkuu wa Vatican wakati wa kuwasilisha ujumbe huu, hivi karibuni hapa mjini Vatican. Anasema, katika Maandiko Matakatifu, mauaji ya kwanza yanafanywa na Kaini kwa kumuua Abeli. Huu ndio utamaduni wa kifo unaoweza kupewa majina mbali mbali kama vile: utoaji mimba, mauaji, kifo laini, njaa au vita.

Hivi ni vitendo vinavyowafanya binadamu kushindwa kutambua kwamba, wao ni ndugu, wameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu na kukombolewa na Yesu Kristo ambaye ni ndugu yao. Kwa njia ya Fumbo la Msalaba alirekebisha ubinadamu uliokuwa unaelemewa mno na dhambi kwa kuwakirimia ukombozi. Baba Mtakatifu Francisko anauliza inakuaje watu kwa kugubikwa mno na ubinafsi wanashindwa kutambua thamani ya udugu?

Je, woga na mashindano yasiyokuwa na msingi ndiyo chanzo cha kushindwa kutambua na kuthamini: udugu, heshima na utu wa binadamu? Udugu kama ambavyo umefafanuliwa na viongozi mbali mbali wa Kanisa kama msingi na njia ya amani unakazia kwa namna ya pekee maendeleo ya mtu mzima: kiroho na kimwili; kwa kutambua kwamba, amani ni kwa ajili ya mafao ya wengi na kwamba, udugu ni njiia muafaka katika mchakato wa mapambano dhidi ya baa la umaskini kama alivyowahi kusema Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto wa kumi na sita.

Baba Mtakatifu Francisko alipokutana na waandishi wa habari kwa mara ya kwanza siku tatu baada ya kuchaguliwa kwake, alisema amechagua kuitwa Francisko wa Assisi: Fukara, mtu wa amani, anayependa na kuthamini mazingira. Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwa Siku ya 47 ya Kuombea Amani Duniani kwa Mwaka 2014 anapembua dhana ya: Umaskini, amani, mazingira mintarafu uelewa wa udugu kati ya watu.

Baba Mtakatifu anasema, katika mchakato wa maboresho ya uchumi kuna haja kwa Jumuiya ya Kimataifa kujikita katika udugu unaoshinda hali ya kutojali wala kuguswa na mahangaiko ya wengine. Ni dhana inayoshinda kinzani, migawanyiko na uadui.Ni changamoto na mwaliko wa kujikita katika mchakato wa kutafuta na kudumisha misingi ya haki na amani duniani pasi na woga wa vita wala matumizi ya silaha za maangamizi pamoja na silaha ndogo ndogo.

Katika chokochoko na kinzani za kijamii, udugu unakuwa ni silaha madhubuti katika mapambano dhidi ya rushwa na ufisadi; uhalifu wa vikundi, utumwa, biashara haramu ya binadamu na utumwa mamboleo mambo ambayo kimsingi yanaharibu tunu msingi za maisha ya binadamu, familia na uchumi katika ujumla wake.

Kardinali Turkson anasema, Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwa ajili ya Siku ya Kuombea Amani, anawahimiza waamini na watu wote wenye mapenzi mema, kusimama kidete kutetea, kulinda na kutunza mazingira, kwa kutambua kwamba, hii ni zawadi ya kazi ya Uumbaji, inayopaswa kufurahiwa na wengi, kwa shukrani na haki.

Kardinali Peter Turkson katika tafakari yake kwa ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko kwa ajili ya Siku ya kuombea Amani Duniani kwa Mwaka 2014 anamwangalia Hayati Mzee Nelson Mandela, aliyefariki dunia hivi karibuni akiwa na umri wa miaka 95. Baada ya miaka 27 ya kufungwa gerezani, Tata Madiba aliibuka na ujumbe wa upatanisho, akataka ukweli kuhusu kurasa chungu za historia ya Afrika ya Kusini zilizopita zifahamike na kukubaliwa. Ukweli na upatanisho, zikawa ni nyenzo msingi za ujenzi wa Afrika ya Kusini mpya, pasi na ubaguzi. Kwa ushuhuda wa maisha na uongozi wake makini, watu wengi wakatubu na kuachana na utamaduni wa kifo.

Baba Mtakatifu Francisko anawachangamotisha waamini na watu wote wenye mapenzi mema kufanya toba na wongofu wa ndani katika hija ya maisha ya kila siku, ili kugundua tena na tena udugu, unaopaswa kumwilishwa na kushuhudiwa kwa njia ya mapendo. Kwa kutambua kwamba, upendo ni zawadi ya Mungu kwa waja wake, inawezekana pia kupokea udugu na kuufanyia kazi.

Kipindi cha Majilio na hatimaye, Maadhimisho ya Siku kuu ya Noeli, ni fursa ya kuanzisha mchakato wa; msamaha, upatanisho na amani, ili hatimaye, kuweza kuadhimisha Siku kuu ya Noeli kwa moyo mpya, kila mtu akijitahidi kuwa ni zawadi kwa jirani yake. Jamii ijitahidi kuwaangalia maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii; kwa kuheshimiana na kuthaminiana kwa kutambua kwamba, binadamu wote ni ndugu!

Na Padre Richard Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.







All the contents on this site are copyrighted ©.