Jubilee ya Miaka 50 ya Uhuru wa Kenya, iwe ni fursa ya kujenga na kuimarisha haki,
umoja, upendo, msamaha na upatanisho!
Maadhimisho ya Jubilee ya Miaka 50 tangu Kenya ilipojipatia uhuru wa bendera ni changamoto
na mwaliko kwa wananchi wote wa Kenya kujikita katika mchakato wa ujenzi wa misingi
ya: haki, umoja na mshikamano wa kitaifa; upendo, msamaha na upatanisho wa kitaifa.
Ni ujumbe unaotolewa na Baraza la Maaskofu Katoliki Kenya wakati huu wananchi
wa Kenya wanapoendelea kumwimbia Mungu utenzi wa sifa na shukrani kwa Jubilee ya miaka
50 tangu walipojipatia uhuru wa bendera.
Padre Vincent Wambugu, Katibu mkuu
wa Baraza la Maaskofu Katoliki Kenya anasema kwamba, Kanisa litaendelea kuwa ni sauti
ya kinabii, inayowahamasisha wananchi kupendana, kuheshimiana, kusaidiana, kusameheana
na kujipatanisha wao kwa wao! Mshikamano na umoja wa kitaifa ni dhamana inayopaswa
kufanyiwa kazi na wananchi wote wa Kenya.
Katika mapambano dhidi ya ukoloni,
watu walipigania uhuru wakajikuta wanakinzana kwa misingi ya kikabila. Jubilee ya
miaka 50 ua Uhuru wa Kenya, iwe ni fursa ya kufanya tafakari ya kina, ili kutambua
mapungufu yaliyojitokeza, tayari kufungua ukurasa mpya!
Mzee Nelson Mandela,
awe ni mfano wa kuigwa katika kujenga misingi ya ukweli, upatanisho na amani. Kenya
sasa inapaswa kujikita katika mikakati na sera za maendeleo endelevu; kwa kuzingatia
misingi ya haki, amani, utawala bora, umoja na mshikamano wa kitaifa. Ni wajibu wa
viongozi wa Kenya kuhakikisha kwamba, wanajikita katika kukuza na kudumisha tunu msingi
za maisha adili, mafao ya wengi, haki na amani.