Askofu Michael Msonganzila wa Jimbo Katoliki Musoma, hivi karibuni alifunga rasmi
Mwaka wa Imani kwa Ibada ya Misa Takatifu iliyofanyika kwenye Kanisa kuu la Bikira
Maria Mama wa Mungu, Musoma. Katika mahubiri yake alikazia mambo makuu matano kuhusu
imani yaani: Imani inapaswa kuadhimishwa, kuuishi, kuilinda, kuitetea na kuieneza.
Askofu Msonganzila katika mahojiano maalum na Radio Vatican anafafanua zaidi vipengele
hivi.
Itakumbukwa
kwamba, Jimbo la Musoma, limeadhimisha Mwaka wa Imani sanjari na Maadhimisho ya Sinodi
ya kwanza ya Jimbo Katoliki Musoma na vikao vya Sinodi bado vinaendelea. Kati ya mada
zilizojadiliwa kwenye kikao cha mwisho kilichofanyika kuanzia tarehe 9 hadi 13 Desemba
2013 ni: Liturujia, Utamadunisho, miito na changamoto zake. Wawezeshaji walikuwa ni
Padre Romuald Kajara na padre Nicholas Segeja.
Ifuatayo ni risala kwa Askofu
Msonganzila iliyotolewa na Padre Valence Matungwa, Mkurugenzi Idara ya Uchungaji,
Jimbo Katoliki Musoma.
Mhashamu Baba Askofu Michael Msonganzila, waheshimiwa
Mapadre, Watawa na Waamini wote Tumsifu Yesu Kristo…. Sinodi Musoma….
Mhashamu
Baba Askofu, tumekusanyika katika Kanisa hili Kuu la Jimbo kwa ajili ya kufunga Mwaka
wa Imani katika ngazi ya Jimbo. Mwaka wa Imani, katika ngazi ya Ulimwengu, ulifunguliwa
tarehe 11 Oktoba 2012 na Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI na kufungwa tarehe 24
Novemba 2013 na Baba Mtakatifu Francisko huko Vatican. Katika ngazi ya Jimbo, Mwaka
wa Imani ulifunguliwa nawe Askofu wetu wa Jimbo tarehe 18 Desemba 2012 hapa hapa katika
Kanisa Kuu.
Mhashamu Baba Askofu, Mwaka wa Imani ulilenga kutoa mwaliko kwa
ajili ya wongofu mpya wa maisha katika Kristo na kutoa fursa ya kuvumbua na kujifunza
misingi ya Imani yetu. Umekuwa ni kipindi cha kuamsha katika kila mwamini hamu ya
kukiri Imani kikamilifu, kwa kujiamini na kwa matumaini ikiwa ni pamoja na kutoa msukumo
mpya kwa utume wa Kanisa zima ili kuwaongoza watu kutoka katika maisha ya giza la
imani na kuwapeleka mahali pa mwanga, uhai na urafiki na Kristo ambaye anatupatia
maisha kamili.
Mhashamu Baba Askofu, kwa namna ya pekee, Mwaka wa Imani umetoa
mwaliko wa kukuza uhusiano binafsi na Mungu. Mwaliko huu wa pekee unatufahamisha kuwa
Imani ambayo ni zawadi ya Mungu kwa Kanisa lake, inahitaji jitihada ya kila mtu binafsi
kuielewa, kuiishi, kuilinda, kuikuza na kuieneza. Kwa jinsi hii, Imani inayopokewa
kama zawadi, inamwajibisha kila mmoja wetu awe ishara hai ya uwepo wa Kristo Mfufuka
pale mahala anapoishi na kufanya kazi.
Ili kutekeleza mwaliko huo, wa kukuza
uhusiano binafsi na Mungu, kila mmoja wetu alialikwa kuzingatia mambo manne kama ifuatavyo;
Ekaristi Takatifu
Kila mmoja wetu amealikwa kushiriki kikamilifu
katika maadhimisho ya kiliturjia hasa Ekaristi Takatifu. Hiki ndicho kilele ambapo
kazi ya Kanisa inaelekea na papo hapo ni chemichemi zimamotoka nguvu zake zote. Ekaristi
Takatifu ni Mkate wa Uzima unaolisha roho zetu na kuziimarisha.
Maungamo
Kila
mmoja wetu amealikwa kudumisha na kutoa msukumo mpya wa kupokea mara kwa mara Sakramenti
ya Upatanisho. Ni katika Sakramenti hii muumini anakutana na Moyo wa Upendo na wa
Huruma wa Mungu Baba. Kanisa ni mlango wa huruma ya Mungu, huruma ambayo inatunyanyua
kutoka katika dhambi na kututia nguvu mpya ya kuendelea na safari ya kuelekea utimilifu
wa Ufalme wa Mungu. Mwaka wa Imani ulimwalika kila mmoja wetu kutambua kuwa Sakramenti
ya Upatanisho ni muhimu sana katika kukuza uhusiano binafsi na Mungu.
Neno la Mungu
Kwa jinsi ile ile tunavyoumega mkate unaolisha
roho zetu na kuziimarisha, vivyo hivyo ni muhimu kulimega Neno la Mungu na kujishibisha
nalo. Mwaka wa Imani umemwalika kila mmoja wetu kuvumbua tena upya hamu ya kujibidisha
kwa Neno la Mungu linaloletwa kwetu kiaminifu kwa njia ya Kanisa.
Ujuzi
wa Imani
Huu ni mwaliko wa kila mmoja wetu kuijua imani yake. Mtakatifu
Anselmo alikiri kuwa Imani yetu ni imani inayoendana na uelewa na ni imani inayotafuta
uelewa (fides querens entellectum). Kwa kuzingatia kuwa Mwaka wa Imani ulienda sambamba
na kumbukumbu ya Miaka 50 tangu kuitishwa kwa Mtaguso wa Pili wa Vatikano na miaka
20 tangu kutolewa kwa Katekisimu ya Kanisa Katoliki, kila mwamini amealikwa kuyaelewa
matini ya Mtaguso huo na ya Katekisimu. Hii ni pamoja na kujifunza na na kuyaelewa
mafundisho ya Imani yanayopatikana katika machapisho mengine ya Kanisa.
Mhashamu
Baba Askofu, katika Jimbo letu la Musoma tumeadhimisha Mwaka wa Imani katika maadhimisho
mawili makubwa ambayo ni Sinodi ya Jimbo na Matembezi ya Sanamu ya Mama Bikira Maria.
Mhashamu
Baba Askofu, Sinodi ya Jimbo letu ilizinduliwa nawe tarehe 19 Mei 2013 na itaendelea
hadi tarehe 3 Oktoba 2014. Adhimisho hili la Sinodi ni tunda la Mwaka wa Imani. Licha
ya kuwa inaadhimishwa katika Mwaka wa Imani, Sinodi yetu inajumuisha malengo yote
ya Mwaka wa Imani katika lengo lake na tena inapanga mikakati ya kudumu ya kuielewa,
kuiishi, kuikuza na kuieneza Imani yetu katika mazingira yetu. Kwa sababu hii, adhimisho
la Sinodi litaendelea kwa mwaka mmoja zaidi hata baada ya kuhitimisha leo Mwaka wa
Imani.
Ni matumaini yetu kuwa kwa njia ya adhimisho la Sinodi, Imani itazidi
kuamshwa katika wanajimbo wote. Pia tunatumaini kuwa kila mmoja wetu atazidi kuukuza
uhusiano wake binafsi na Mungu kwa njia ya ushiriki mkamilifu katika maadhimisho ya
Ekaristi, Kitubio, Neno la Mungu na katika kuyajifunza mafundisho ya Imani. Kwa wachungaji,
tunatumaini kuwa adhimisho la Sinodi litawaongezea ari ya kichungaji katika kuzidi
kuifundhisha na kuieneza Imani.
Mhashamu Baba Askofu, adhimisho la pili katika
Mwaka wa Imani lilikuwa ni matembezi ya Sanamu ya Mama Bikira Maria. Kwa kutambua
nafasi ya Mama yetu katika safari ya Imani na kwa kuzingatia kuwa Mama huyu ndiye
Msimamizi wa Jimbo letu, tulifanya matembezi hayo katika Jimbo zima. Matembezi hayo
yalianzia parokiani ya Komuge (21 Aprili 2013) Dominika ya Kuombea Miito na kuhitishwa
katika Kanisa Kuu (21 Novemba 2013) siku ya kutolewa Bikira Maria Hekaluni.
Matembezi
yalifanyika kama ifuatavyo;
Udekano wa Rorya 21 Aprili hadi 02
Julai 2013 Udekano wa Tarime 03 Julai hadi 13 Agosti Udekano wa Serengeti 14
Agosti hadi 14 Septemba Udekano wa Butiama 15 Septemba hadi 08 Oktoba Udekano
wa Musoma 09 Oktoba hadi 21 Novemba.
Matembezi haya yamefika katika kila
parokia, kila jumuiya na kila kaya ya Wakatoliki. Ni jambo la kutia moyo kwamba hata
kaya za wasio wakatoliki ziliomba kupitiwa na Sanamu ya Mama Bikira Maria. Pamoja
na maadhimisho hayo katika ngazi ya Jimbo, kila parokia ilikuwa na matukio na maadhimisho
mahalia.
Mhashamu Baba Askofu, tunamshukuru Mwenyezi Mungu kwa neema nyingi
alizotujalia katika maadhimisho hayo ya Mwaka wa Imani. Tunaomba ajalie ili mwamko
wa Imani tulioupata kwa maadhimisho haya uendelee kuwa ndani yetu daima.
Aidha
tunawashukuru wote waliopanga na kufanikisha matembezi ya Sanamu ya Mama yetu Bikira
Maria katika ngazi ya Jimbo na kusimamia utekelezaji wake mpaka ngazi ya Jumuiya NdogoNdogo.
Shukrani za pekee ziwaendee Mapadre, Watawa, viongozi wa Parokia, Jumuiya na Vyama
vya Kitume, wahamasishaji, wote ambao kwa majitoleo yao mbalimbali matembezi hayo
yamefanikiwa.
Tunaendelea kuomba ushirikiano katika maadhimisho ya Sinodi yanayoendelea
ili nayo yaweze kukamilika kadiri ya mipango na matarajio yetu.
Mhashamu Baba
Askofu, baada ya maneno hayo, napenda sasa kukualika utuongoze katika Misa hii Takatifu
ya Kuhitimisha Mwaka wa Imani Kijimbo