2013-12-13 07:18:48

Tafakari ya Neno la Mungu, Jumapili ya tatu ya Kipindi cha Majilio Mwaka A wa Kanisa


Mpendwa msikilizaji wa kipindi tafakari masomo Dominika, ninafurahi tena kuwa nawe katika safari yetu ya Majilio tukijiandaa kwa ajili ya ujio wa Mwana wa Mungu. Ni wakati huu tunapoimba kwa furaha Masiha wetu njoo, ukatuokoe. RealAudioMP3
Tuko sasa Dominika ya tatu ya Kipindi cha Majilio ambapo Neno la Mungu linatualika kutambua kwa njia ya imani alama zinazomtambulisha Masiha. Tunapata kutafakari katika Injili juu ya wasiwasi wa Yohane Mbatizaji juu ya Masiha, kiasi kwamba anatuma wafuasi wake tokea gerezani wakamwulize Bwana wakisema, eti wewe ndiye Masiha tuliyemtarajia au tumngojee mwingine?
Yohane Mbatizaji anaingiwa na wasiwasi kwa sababu aliweka matumaini yake katika alama zisizo za kweli! Kwetu sisi yaweza tokea na inatokea mara kadhaa kutumaini katika bwana asiye mwenyewe! Kumbe leo mwaliko ni huo, yaani kuwa makini ili tusianguke katika mtego kama huo!
Mpendwa msikilizaji, alama ambazo zilisadikika na Yohane Mbatizaji na wafuasi wake ni kuwa Masiha ajaye atakuwa hakimu mkali atakayewapatiliza mbali wadhambi. Kinyume chake Masiha hafanyi hilo isipokuwa upendo kwao akitafuta kuwaokoa katika taabu yao hiyo. Mpendwa msikilizaji, kazi na wajibu wetu mkuu, ni kutambua wakati huo tukijiuliza daima, ni alama zipi zinazomtambulisha Masiha ambaye tunaimba kwa furaha tukisema uje kutuokoa!
Ndiyo kusema, alama za kweli tunazipata katika Somo la kwanza toka kitabu cha Nabii Isaya 35:1-6,10 akisema ndipo vipofu na viziwi watakapoona na kusikia, mwenye kupooza atarukaruka tena na bubu kuimba kwa furaha. Mara moja toka katika alama hizi tunagundua kuwa Masiha anakuja kwa ajili ya kuwaondoa walio katika taabu na kuwaweka huru. Taabu kwa kawaida ni tokeo la dhambi, yawezekana dhambi ya mtu binafsi lakini hasa dhambi kwa ujumla.
Mpendwa msikilizaji, katika hili tunaalikwa kuingia katika safari ya toba na uaminifu kwa Injili kama tusomavyo katika Injili ya Marko. 1:15. Katika toba na kuishi Injili tunafikia kwa namna ya pekee kabisa hatua ya kutambua alama zinazomtambulisha Masiha.
Jukumu la kuishi alama hizi linatuweka katika mazingira ya furaha na linatuonesha waziwazi kwamba utawala wa Masiha unaanza kukolea katika maisha yetu.
Mpendwa mwana wa Mungu, inawezekana ikajitokeza kukawa na kuchelewa katika utekelezaji, yaani kuishi toba na hivi tukaweza kukata tamaa, basi Mtume Yakobo anatutia moyo na tumaini akisema, kuweni na subira mpaka Bwana atakapokuja. Katika subira tunataka polepole kutenganisha uovu na ubaya ulio katika jumuiya na katika mtu awaye yote katika ubinafsi wake.
Katika subira Mtume Yakobo anatuonya daima kuachana na tabia ya kuhukumiana maana hakimu mwaminifu ni mmoja yaani Mfalme Masiha. Mtume Yakobo anatuonya katika subira kutambua kuwa safari ya wokovu lazima itazamwe kama mkulima anavyongojea mvua za masika na za vuli.
Mpendwa msikilizaji, kipindi cha Majilio ni kipindi cha neema, ni kipindi cha kupanda ili kujipatia mavuno hapo baadaye, na kwa hakika mavuno ni furaha ya moyo inayokamilishwa katika Yesu Kristu mfufuka ambaye atatufufua siku ya mwisho na kukaa naye katika kiti cha enzi pamoja na Baba mbinguni.
Nikikutakia majilio njema napenda kusema fikiria zaidi kuwalisha maskini na kuwahudumia wagonjwa katika jumuiya yako na jitahidi kuwa adui wa dhambi kila siku ya maisha yako. Mpendwa, hiyo ndiyo namna ya kuishi Majilio ya mwaka huu. Nakukumbusha tena hapo jirani kwako kuna mtoto ambaye amekosa ada ya shule msaidie na mfundishe namna ya kuitumia na zawadi yako kwa hakika ni mbinguni. Tumsifu Yesu Kristo na Bikira Maria.

Tafakari hii imeletwa kwako na Padre Richard Tiganya, C.PP.S.









All the contents on this site are copyrighted ©.