Baba Mtakatifu Francisko ameteuliwa na Gazeti maarufu la TIME kuwa ni mtu mashuhuri
kwa Mwaka 2013. Akizungumzia uteuzi huu, Padre Federico Lombardi, msemaji mkuu wa
Vatican anabainisha kwamba, Vatican kwa ujumla hakushangazwa na uteuzi huu, kwani
kuna vielelezo makini vinavyoonesha mguso na mashiko tangu Baba Mtakatifu Francisko
achaguliwe kuliongoza Kanisa Katoliki kama Khalifa wa Mtakatifu Petro.
Padre
Lombardi anasema, hili ni jambo jema kuona kwamba, hata magazeti ya kimataifa yameona
na kutambua mchango wa Baba Mtakatifu Francisko, mtu ambaye kimsingi anapenda kujikita
katika tunu msingi za maisha ya kiroho, kidini, maadili na utu wema. Baba Mtakatifu
Francisko ameendelea kujipambanua kwa kuwa ni sauti ya wanyonge ndani ya Jamii, kiongozi
anayetetea misingi ya haki, amani, upendo na mshikamano wa kidugu.
Padre Lombardi
anakumbusha kwamba, Papa Francisko si mtu anayependa kujikuza wala kupewa sifa, kwani
yote anayotenda ni sehemu ya mchakato wa maisha na dhamana yake ya kutangaza Injili
ya Furaha, Upendo bna Huruma ya Mungu kati ya Watu wa Mataifa. Ikiwa kama mambo haya
yanaleta mvuto, mashiko na matumaini kwa watu, basi Baba Mtakatifu Francisko anayo
sababu ya kuridhika na kumshukuru Mungu. Lakini Baba Mtakatifu Francisko atafurahi
zaidi ikiwa kama walau watu wameufahamu ujumbe na nia yake.