2013-12-13 07:37:43

Jengeni na kudumisha utandawazi wenye mshikamano wa huduma makini kwa wagonjwa!


Mkutano wa ishirini na nane ulioandaliwa na Baraza la Kipapa kwa ajili ya shughuli za kichungaji kwa wafanyakazi katika sekta ya afya, uliohitimishwa hivi karibuni hapa mjini Vatican, umetoa changamoto kwa Jumuiya ya Kimataifa kuhakikisha kwamba, huduma ya afya inajikita katika utandawazi wenye mshikamano, utandawazi unaoguswa na mahangaiko ya wagonjwa hata wale waliokufani, kwani wao pia wanahitaji kuonja huruma na msaada kutoka kwa wengine. RealAudioMP3

Ni huduma ambayo inapaswa kutolewa kwa kuzingatia kanuni maadili, sheria, utu na maisha ya binadamu.

Itakumbukwa kwamba, mkutano huu, ulikuwa unaongozwa na kauli mbiu “Kanisa katika huduma kwa wazee wagonjwa: tiba kwa wagonjwa wenye matatizo ya mishipa ya fahamu” Askofu mkuu Zygmunt Zimowski, Rais wa Baraza la Kipapa kwa ajili ya shughuli za kichungaji kwa wafanyakazi katika sekta ya afya anabainisha kwamba, mkutano huu umehudhuriwa na idadi kubwa ya wajumbe wapatao 700 kutoka katika nchi 57.

Ni watu waliotoka katika medani mbali mbali za maisha ya mwanadamu: kiuchumi, kisiasa na kitamaduni. Wameshirikishana, ujuzi, mang’amuzi, wasi wasi na vipaumbele vyao kwa ajili ya huduma kwa wagonjwa mahali popote pale walipo. Ni mkutano ambao umewashirikisha pia wajumbe waliokuwa na imani na dini tofauti, lakini wote kwa pamoja wamemwangalia mgonjwa, aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu.

Mkutano huu umekuwa ni jukwaa la majadiliano ya kina, kama ambavyo anaendelea kukazia Baba Mtakatifu Francisko kama sehemu ya mchakato wa kuwatangazia watu Injili ya Furaja, ili kuweza kukua na kukomaa kwa kuwasikiliza wengine. Utu na heshima ya binadamu hata pale wanaokuwa wanateseka na kushambuliwa na magonjwa, bado wanapaswa kuheshimiwa na kuthaminiwa.

Wajumbe wamepinga kwa kauli moja utamaduni wa kifo na badala yake, wanaendelea kuhimiza waamini na watu wenye mapenzi mema kujikita zaidi katika kutangaza Injili ya Uhai, dhidi ya sera zinazokumbatia utamaduni wa kifo. Wajumbe wamekubaliana kimsingi kwamba, hata pale sera za kifo laini zinapotangazwa na kuonekana kana kwamba, ni huruma kwa wagonjwa, lakini hapa kinachopewa msukumo zaidi ni masuala ya uchumi na wala si utu na heshima ya binadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Haya ni machozi ya mamba! Hapendwi mtu, ila pochi ndiyo inayotafutwa kama wanavyosema Waswahili wa Pwani!

Gharama za tiba zinaendelea kupanda siku hadi siku kutokana na kuongezeka kwa umri wa watu kuishi na waathirika wakubwa ni wazee. Shirika la Afya Duniani, WHO linasema, kuna haja ya kuwa na mikakati makini ya huduma za afya kwa waathirika wa magonjwa ya mishipa ya fahamu. Kwa sasa wagonjwa hawa wamefikia millioni 35. Inakadiriwa kwamba, ifikapo mwaka 2050 wagonjwa hawa watakuwa wamefikia millioni 100.

Kumbe, kuna haja ya kujenga utamaduni wa mshikamano katika utandawazi unaoguswa na mahangaiko ya watu, ili kuwajengea matumaini ya kuweza kupona. Ni mshikamano unaopaswa kufanywa na wadau mbali mbali katika sekta ya afya na Kanisa lina uwezo mkubwa wa kuhamasisha jambo hili. Magonjwa mengi yanayotokana na uzee yanaweza kupatia tiba kwenye nchi zilizoendelea, lakini jambo la msingi ni kuhakikisha kwamba: kanuni, maadili, utu na heshima na maisha yabinadamu yanapewa kipaumbele cha kwanza.

Askofu mkuu Zymunt Zimowski anasema, utandawazi wa huduma ya afya unaojali, ni jambo linalowezekana, kwa ajili ya wagonjwa wenye kuhitaji tiba na huduma, ikiwa kama watu watatekeleza wajibu na dhamana ya kulinda na kutetea Injili ya Uhai.








All the contents on this site are copyrighted ©.