Bado Wakristo wanaendelea kudhulumiwa hata katika nchi zile zinazodhani kuwa zina
demokrasia ya kweli!
Askofu mkuu Dominique Mamberti, Katibu mkuu wa mambo ya nchi za nje na ushirikiano
wa kimataifa mjini Vatican, hivi karibuni ameshiriki katika mkutano wa ishirini wa
Mawaziri wa ulinzi na usalama na ushirikiano wa kimataifa kutoka katika nchi za Ulaya,
OSCE, uliokuwa unafanyika mjini Kiev, Ukraine kwa kusema kwamba, Wakristo wanadhulumiwa
na kunyanyaswa hata kwenye nchi zile ambazo zina demokrasia.
OSCE katika
kipindi cha miaka kumi iliyopita imejitahidi kutekeleza wajibu wake kikamilifu hasa
katika masuala ya udhibiti wa silaha na sera za kijeshi. Ujumbe wa Vatican umeonesha
kutoridhika kwake kutokana na kusuasua kwa utekelezaji wa Hati ya Vienna, inayokazia
ukweli na uwazi kuhusu masuala ya kijeshi sanjari na amani na utulivu kwa nchi wanachama.
Askofu
mkuu Mamberti, akizungumzia kuhusu uchumi na mwelekeo wake katika utunzaji bora wa
mazingira, amezitaka nchi wanachama kuonesha utashi wa kisiasa katika mchakato unaopania
kulinda na kutunza mazingira, sanjari na matumizi bora ya nishati rafiki kwa ajili
ya maendeleo ya wengi.
Wajumbe wa OSCE wamejadili pia kuhusu tatizo la wakimbizi
na wahamiaji Barani Ulaya. Ujumbe wa Vatican kwenye mkutano huu umekazia umuhimu wa
kulinda na kudumisha haki msingi za wakimbizi na wahamiaji, hata wakati huu nchi nyingi
za Ulaya zinapokabiliana na athari za myumbo wa uchumi kimataifa. Wahamiaji wasiangaliwe
tu kama nguvu kazi ya mpito, bali raia wenye utu, haki na wajibu wa kutekeleza katika
jamii inayowpatia hifadhi.
Askofu mkuu Mamberti anasema, biashara haramu ya
binadamu ni jambo ambalo linaendelea kuongezeka kwa kasi kubwa duniani, kumbe, kuna
haja kwa Jumuiya ya Kimataifa kulivalia njuga tatizo hili linalodhalilisha utu na
heshima ya binadamu. Mwelekeo na mwono sahihi wa binadamu; uhuru wa dhamiri na wa
kidini ni kati ya mambo nyeti yaliyojadiliwa na wajumbe wa mkutano wa OSCE. Inasikitisha
kuona kwamba, hata baada ya karne kumi na saba za uhuru wa kidini Barani Ulaya, kuna
baadhi ya mataifa ambayo yanaendeleza dhuluma na nyanyaso za kidini dhidi ya Wakristo.