2013-12-12 09:41:07

Uzalendo kwanza na wala msitafute madaraka ili kujipatia sifa na utajiri!


Baraza la Maaskofu Katoliki Madagascar, katika ujumbe wake wa kufunga Mwaka wa Imani na Jubilee ya Miaka 75 tangu Biblia ilipotafsiriwa kwa mara ya kwanza katika lugha ya Kimalagascia, wanawaomba wagombea uchaguzi mkuu nchini humo, kuhakikisha kwamba, wanatoa kipaumbele cha kwanza kwa mafao ya wengi, haki, amani, ustawi na maendeleo ya wananchi wa Magadascar na wala si kutaka kukimbilia vyeo na heshima!

Maaskofu wanawataka wagombea kiti cha urais nchini humo kuonesha moyo wa uzalendo na ukomavu wa kisiasa kwa kutaka kusimama kidete kulinda na kutetea masilahi ya taifa na kamwe wasiwe vibaraka wa watu kutoka nje wanaoweza kuwatumia kwa ajili ya mafao yao binafsi. Watambue kwamba, Madagscar ni mali ya wananchi wa Madagascar na wala si bidhaa inayoweza kuuzwa kwa utashi wa wanasiasa wa Madagascar.

Tarehe 20 Desemba 2013 wananchi wa Madagascar watafanya uchaguzi mkuu kuchagua kati ya: Jean Louis Robinson aliyepata asilimia 21.10% na Bwana Hery Rajoanarimampianina aliyejipatia wastani wa 15.93 ya kura zote zilizopigwa hivi karibuni nchini Madagascar.

Maaskofu wanasikitika kusema kwamba, kuna baadhi ya wanasiasa wanaokimbilia madaraka kwa ajili ya kujitafutia umaarufu na utajiri wa haraka haraka na kusahau kwamba, uongozi ni huduma; matokeo yake ni kwamba, baadhi ya wanasiasa wanapoingia madarakani wanajikuta wanaandamwa na vitendo vya ufisadi, wizi na rushwa pamoja na mmong'onyoko wa maadili na utu wema.

Maaskofu wanaitaka Jumuiya ya Kimataifa kusimama kidete kulinda na kuwatetea wanyonge badala ya kuendelea kuwa ni watazamaji wasiokuwa na msaada wakati taifa linakabiliana na majanga pamoja na kinzani. Nchi ya Madagascar inaandamwa kwa rushwa, kinzani na migogoro ya kijamii, ukosefu wa amani na utulivu pamoja na uharibifu mkubwa wa mazingira. Kuna pengo kubwa kati ya matajiri na maskini wanaolala wakiwa macho wazi kama bundi!

Utawala wa sheria unaonekana kumong'onyoka taratibu kiasi cha watu kuanza kujichukulia sheria mkononi! Ukabila unaanza kutawala kiasi cha kuwafanya wananchi wa Madagascar waanze kunyoosheana vidole, hali ambayo ni hatari kwa umoja na mshikamano wa kitaifa.

Ni matumaini ya Baraza la Maaskofu Katoliki Madagascar kwamba, kiongozi atakayechaguliwa hapo tarehe 20 Desemba 2013, atajitahidi kuwa ni kiongozi wa wananchi wote wa Madagascar; tayari kuponya madonda ya chuki na utengano, ili kuimarisha umoja na mshikamano wa kitaifa; utawala wa sheria na mafao wengi. Jamii inapaswa kujifunza kutekeleza wajibu wake barabara na kwamba, matumizi ya nguvu si mtaji wa maendeleo ya watu.

Wananchi wajenge na kuimarisha utamaduni wa kupenda na kusimamia ukweli, haki na amani; wasimame kidete kutetea Injili ya Uhai na kupinga rushwa kwa nguvu zao zote kwani hili ni janga la kitaifa. Kutokana na rushwa na ufisadi uliokuwa umekithiri nchini Madagascar, Benki ya Afrika imeamua kupunguza msaada wake kwa kipindi cha miaka miwili, yaani kuanzia mwaka 2014 hadi mwaka 2016, jambo ambalo litaleta madhara makubwa kwa wananchi wa Madagascar.







All the contents on this site are copyrighted ©.