Maandalizi ya Siku ya Vijana Duniani kwa Mwaka 2016 yaanza kutimua vumbi!
Kardinali Stanislaw Dziwisz, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Krakovia, Poland, hivi karibuni
ametangaza kwamba, kuanzia tarehe 25 Julai hadi tarehe Mosi Agosti 2016, Jimbo kuu
la Krakovia, litakuwa linaadhimisha Siku ya 31 ya Vijana Duniani inayoongozwa na kauli
mbiu “Heri wenye rehema maana hao watakuwa na rehema. Mt. 5:7.
Maadhimisho
haya ni uamuzi uliotolewa na Baba Mtakatifu Francisko mara baada ya Maadhimisho ya
Siku ya 28 ya Vijana Duniani kwa Mwaka 2013 yaliyofanyika mjini Rio de Janeiro, nchini
Brazil.
Vijana kutoka kona mbali mbali za dunia, watafika na kushuhudia mahali
alipozaliwa, akaishi na kulitumikia Kanisa kama Padre, Askofu na hadi pale alipochaguliwa
kuwa Khalifa wa Mtakatifu Petro. Hili ni tukio la kimataifa litakalokuwa ni mwendelezo
wa Maadhimisho ya sherehe na shamra shamra baada ya Mama Kanisa kumtangaza Mwenyeheri
Yohane Paulo II kuwa Mtakatifu hapo tarehe 27 Aprili 2014.
Vijana wengi wameonesha
nia na hamu ya kushiriki kwa mara nyingine tena katika tukio hili la kiimani ambalo
limekuwa ni la pekee katika maisha na utume wa Mama Kanisa kwa vijana. Tayari Jimbo
kuu la Krakovia limekwisha anzisha tovuti inayoendelea kusimulia maandalizi ya Maadhimisho
ya Siku ya 31 ya Vijana Duniani kwa Mwaka 2016.
Baba Mtakatifu Francisko tayari
amekwisha toa kauli mbiu ya Maadhimisho ya Vijana Kijimbo la Kimataifa kuanzia mwaka
2014 hadi Mwaka 2016. Kwa wale wanaopenda kujihabarisha zaidi wanaweza kufuatilia
habari hizi kwenye mtandao wa Jimbo kuu la Krakovia kwa ajili ya Maadhimisho ya Siku
ya Vijana Duniani kwa Mwaka 2016 kwa anuani ifuatayo: krakow2016.com
Kama
kawa! Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican kwa njia ya mtandao wake itaendelea kukujuza
yale yanayojiri kuhusiana na maandalizi haya; ukiona inapendeza mshirikishe jirani
yako pia, kwani mambo mazuri ni kushirikishana!