Tata Madiba, kwa heri! Umekuwa ni daraja la upatanisho kati ya watu wa mataifa!
Mwili wa Marehemu Nelson Mandela, Siku ya Jumatano tarehe 11 Desemba 2013 umewasili
mjini Pretoria ambako utakaa kwa muda wa siku tatu, ili kutoa nafasi kwa wananchi
wa Afrika ya Kusini kutoka heshima zao za mwisho. Magari ya Polisi yaliusindikiza
Mwili wa Tata Madiba kutoka kwenye Hospitali ya Kijeshi.
Maelfu ya watu yalijipanga
barabarani kumpungia mkono Tata Madiba anapoelekea kwenye nyumba yake ya mwisho hapa
duniani, huko Qunu, Kijijini kwake na hatimaye, kukamilisha hija ya maisha yake hapa
duniani, Jumapili tarehe 15 Desemba 2013.
Kati ya matukio makubwa yatakayokumbukwa
na Jumuiya ya Kimataifa wakati viongozi wakuu wa Jumuiya ya Kimataifa walipoungana
na wananchi wa Afrika ya Kusini kutoka heshima zao za mwisho kwa Mzee Nelson Mandela,
mtu wa watu ni kitendo cha Rais Barack Obama wa Marekani kuonana uso kwa uso na hatimaye
kushikana mkono na Rais Raul Castro wa Cuba, kitendo ambacho hakijawahi kutokea baina
ya wakuu wa nchi hizi mbili, takribani miaka 50 iliyopita. Ndiyo maana Tata Madiba
anakumbukwa na wengi kama daraja la upatanisho kati ya maadui, changamoto ya kuendeleza
hazina hii kubwa kati ya watu wa mataifa.
Tarehe 10 Desemba 2013, ilikuwa siku
muhimu sana kwa wananchi wa Afrika ya Kusini, siku ambayo: umati wa watu kutoka sehemu
mbali mbali za dunia, umesimama kuomboleza kifo cha Tata Madiba. Marais, mawaziri
wakuu, Maspika wa mabunge na raia wa kawaida, walifika kwenye Uwanja wa michezo ulioko
Johannesburg, ili kutoa heshima zao za mwisho. Baadhi ya viongozi hawa wameshangiliwa
na wengine kuzomewa! Kardinali Peter Turkson, Rais wa Baraza la Kipapa la haki na
amani, alikuwepo jukwaani kumwakilisha Baba Mtakatifu Francisko katika tukio hili
la kihistoria.
Ilikuwa ni kumbu kumbu ya Miaka 20 tangu Mzee Nelson Mandela
na Bwana F.W. de Klerk, walipotunukiwa tuzo ya amani, kwa Jumuiya ya Kimataifa kutambua
jitihada zao za pamoja katika kusitisha utawala wa ubaguzi wa rangi. Viongozi ambao
baadaye, walijenga na kuimarisha urafiki wa dhati kati yao! Bwana Klerk, alikuwepo
pia uwanjani, kutoa heshima zake za mwisho kwa Tata Madiba!
Katibu mkuu wa
Umoja wa Mataifa, Bwana Ban Ki-Moon, ameusifu mchango wa Mzee Nelson Mandela katika
mchakato wa upatanisho wa kitaifa. Hakumchukia mtu, bali alichukia chuki na uhasama
kati ya watu, akaonesha nguvu ya kusamehe na kusahau. Mzee Madiba ameiachia Jumuiya
ya Kimataifa urithi mkubwa ambao ni kama mti mkubwa uliozamisha mizizi yake katika
fikira na mioyo ya watu.
Rais raul Castro amegusia uhusiano wa kirafiki uliokuwepo
kati ya Mzee Nelson Mandela na Rais Fidel Castro wa Cuba; watu waliosimama kidete
kulinda na kutetea utu na heshima ya binadamu; haki, uhuru na demokrasia ya kweli.
Mzee Madiba atakumbukwa na wengi kwa kuwa ni "Nabii wa Umoja wa kitaifa, upatanisho
na haki".
Rais Barack Obama wa Marekani aliyekuwa anashangiliwa na wengi kutokana
na ushuhuda wake kuhusu maisha na changamoto alizopata kutokana na kumfahamu Mzee
Nelson Mandela, anasema, Tata Madiba ni kati ya wanasiasa mashuhuri wa Karne ya ishirini
na moja, aliyediriki kuwashirikisha wengine wasi wasi, mahangaiko yake ya ndani, mahesabu
yake tenge na ushindi mkubwa aliofanikiwa kujipatia wakati wa maisha yake hapa duniani.
Mzee Madiba amekuwa ni sauti ya wanyonge; mtu aliyekazia tunu msingi za maisha
ya kimaadili, haki na amani. Itakuwa ni vigumu kwa dunia kumpata Mandela mwingine.
Rais Obama amewataka vijana wa Afrika ya Kusini na vijana wengine wote popote pale
walipo, kuhakikisha kwamba, wanajitahidi kujichotea hazina kubwa iliyoachwa na Mzee
Nelsona Mandela.
Rais Jacob Zuma amemwelezea Mzee Madiba kuwa ni kiongozi jasiri
aliyejitosa kimasomaso kwa ajili kulinda na kutetea uhuru wa wote. Ni kiongozi ambaye
maisha yake yameacha chapa ya kudumu katika watu wa Mataifa. Serikali ya Afrika ya
Kusini itaendelea kuenzi mchango mkubwa wa Tata Madiba katika maisha na ustawi wa
wananchi wa Afrika ya Kusini kwa kukazia: demokrasia, utu na heshima ya binadamu;
kuendeleza mchakato wa mapambano dhidi ya umaskini, baa la njaa, ujinga, maradhi na
ukosefu wa fursa za ajira.
Mwakilishi wa Familia ya Mzee Mandela. Jenerali
Thanduxolo Mandela amesema kwamba, wanatambua kwamba, Mzee Madiba alikuwa ni mtu wa
watu si tu kwa ajili ya Familia yake, Afrika ya Kusini, bali ni mtu aliyejitoa kwa
ajili ya ustawi na maendeleo ya Afrika na Ulimwengu katika ujumla wake.
Askofu
mkuu mstaafu Desmond Tutu, amewataka viongozi na wananchi wa Afrika ya kusini kuwa
na nidhamu kama njia ya kumuenzi Mzee Nelson Mandela, aliyefariki dunia akiwa na umri
wa miaka 95; maisha ambayo ameyasadakisha kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya wananchi
wa Afrika ya Kusini.
Viongozi wengine waliobahatika kuhutubia ni pamoja na
Rais Dilma Rousseff kutoka Brazil, Bwana Li Yuanchao, Makamu wa Rais wa China, Bwana
Hifikepunye Pohamba, Rais wa Namibia pamoja na Bwana Pranab Mukherjee, Rais wa India.