Rushwa ni adui wa haki na ina madhara makubwa sana katika uchumi wa dunia. Inakadiriwa
kwamba, rushwa inayotembea na kutembezwa duniani ni sawa na asilimia 10% ya Pato Ghafi
la Dunia. Hizi ni takwimu zilizotolewa na Umoja wa Mataifa katika Maadhimisho ya Siku
ya Kimataifa ya kupambana na rushwa ya kijamii, kisiasa na kiuchumi iliyofanyika hapo
tarehe 9 Desemba 2013.
Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Bwana Ban Ki-Moon
katika ujumbe wake kwa maadhimisho haya anasema "rushwa ni janga la kimataifa" inayojionesha
si tu katika biashara na matumizi haramu ya dawa za kulevya na silaha, kwa sasa rushwa
imepenyeza mizizi yake katika masuala ya uchumi, mazingira, katika huduma za kiafya
na maliasili.
Rushwa inakwamisha ukuaji chanya wa uchumi kwa kuongeza gharama
za uzalishaji na vitisho; inahatarisha haki msingi za binadamu na kuongeza baa la
umaskini wa hali na kipato kati ya watu wa mataifa; ni janga ambalo linachangia kukua
na kupanuka kwa pengo la wenye nacho na "akina yakhe pangu pakavu, tafadhali tia mchuzi"!
Hii ni fedha na rasilimali ambayo ingechangia kuleta maboresho ya huduma za
elimu, afya na maendeleo ya jamii, lakini kwa bahati mbaya zinaishia mikononi mwa
watu wachache, wenye uchu wa mali na madaraka.
Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa
anasema kwamba, rushwa inaendelea kusababisha majanga makubwa kwa ustawi na maendeleo
ya watu duniani. Rushwa katika huduma za afya inakadiriwa kwamba, inagharimu kiasi
cha dolla za kimarekani billioni 12 hadi 24 kwa Mwaka.