2013-12-10 08:04:23

Waonjesheni maskini moyo wa huruma na mapendo kwa kuchangia kwenye Benki ya Chakula!


Askofu mkuu Justin Welby wa Jimbo kuu la Canterbury na Kiongozi mkuu wa Jumuiya ya Kiangalikani, anawasihi waamini na watu wote wenye mapenzi mema wakati huu wa Maandalizi ya Kipindi cha Noeli, kuonesha moyo wa huruma, upendo na mshikamano kwa maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii kwa kuchangia walau katika Benki ya Chakula, badala ya kupenda mno raha na starehe. RealAudioMP3
Ushauri huu unakuja wakati ambapo takwimu zinaonesha kwamba, idadi ya maskini wa hali na kipato chini Uingereza inaendelea kuongezeka maradufu.
Wananchi wakichangia kwenye Benki ya Chakula, watasaidia baadhi ya watu kupata walau chakula badala ya kutumia fedha nyingi kwa ajili ya kununulia zawadi, mavazi, chakula na vinywaji, mambo ambayo yanaonekana kuwa ya kawaida wakati wa shamrashamra za Noeli na Mwaka Mpya.
Askofu mkuu Justin Welby anawataka waamini na watu wenye mapenzi mema waliobahatika kuwa na uwezo wa kiuchumi kuhakikisha kwamba, wanatumia vyema mali waliyo nayo kwa hekima, busara na maadili na kamwe mali isiwe ni chanzo cha kufilisika kimaadili na utu wema. Takwimu za kiuchumi zinaonesha kwamba, wananchi wa Uingereza wataongeza matumizi maradufu katika zawadi, ikilinganishwa na mwaka 2012, ingawa watu wengi bado wanachechemea kutokana na athari za myumbo wa uchumi kimataifa.
Serikali ya Uingereza kwa siku za hivi karibuni imeendelea kupunguza ruzuku kwa huduma za kijamii kiasi kamba, familia nyingi zinajikuta zikiteseka kwa ukata wa maisha. Malipo ya umeme yameongezeka hali ambayo inazifanya familia nyingi kujikuta ziko njia panda anasema Askofu mkuu Justin Welby. Familia maskini hazina budi kusaidiwa kwa njia ya vyama vya mikopo, ili kuzijengea uwezo wa kiuchumi.
Kutokana na kuongezeka kwa umaskini, baadhi ya Wasamaria wema nchini Uingereza, wameanzisha maduka ya mshikamano wa upendo, kwa kuuza bidhaa kwa bei nafuu. Kwa mara ya kwanza tangu Vita kuu ya Pili ya Dunia ilipohitimishwa, wananchi wengi wa Uingereza wameanza kuonja makali ya umaskini wa hali na kipato. Makanisa yameanza kuonesha upendo na mshikamano kwa kuanzisha Benki za Chakula!








All the contents on this site are copyrighted ©.