Ukisikia watu wanapiga vigelegele, hapo tambua kuna mtu anajisadakisha!
Watawa watatu wa Shirika la Mapendo, maarufu kama Rosmini, Jumatatu tarehe 9 Desemba
2013 wameweka Nadhiri za daima, kwenye Ibada ya Misa Takatifu iliyoongozwa na Padre
Vito Nardin, kwenye Kanisa kuu la Giovanni Porta Latina, lililoko mjini Roma na kuhudhuriwa
na idadi kubwa ya Mapadre na Watawa kutoka: India, Tanzania na Kenya.
Watawa
wa Shirika la Mapendo kwa njia ya nadhiri za daima wameimarisha ndani mwao neema na
baraka walizojaliwa na Roho Mtakatifu wakati wa Ubatizo, tayari kumwilisha Sheria
za Warosmini katika safari ya maisha na utume wao kama Wanashirika, huku wakikumbatia
Mashauri ya Kiinjili, yaani: Utii, Useja na Ufukara. Injili ya Kristo na Sheria za
Shirika kwa sasa ndio mwongozo makini wa maisha yao kwa ajili ya huduma kwa Mungu
na jirani.
Padre Vito Nardin katika mahubiri yake, amewapongeza watanzania
waliokuwa wanaadhimisha Miaka 52 tangu walipojitwalia Uhuru wa bendera kutoka kwa
Mwingereza na Wakenya wanaposherehekea Jubilee ya Miaka 50 tangu walipojipatia uhuru
wao. Watawa wa Shirika la Mapendo wamekumbushwa kwamba, wanapaswa kuwa tayari kutumwa
na Kristo mahali na wakati wowote na kwa maisha yao yote!
Watawa hawa wameweka
nadhiri za daima baada ya kukamilisha kipindi cha majiundo na malezi mintarafu sheria,
kanuni na maagizo ya Mama Kanisa. Kwa sasa wako tayari kuonesha utii kwa Mwenyezi
Mungu, wakiendelea kushibishwa kwa adhimisho la Fumbo la Ekaristi Takatifu, ili kuzima
kiu ya maisha ya ndani, tayari kukumbatia Mashauri ya Kiinjili.
Padre Nardin
amekumbusha kwamba, maisha ya kitawa ni kielelezo cha hali ya juu cha utii kwa Mwenyezi
Mungu, kwa ajili ya kutangaza Habari Njema ya Wokovu hadi miisho ya dunia. Watawa
katika maisha yao ya kila siku, wanapaswa kuwa ni mashahidi wanaoleta changamoto chanya
ya maisha mapya kwa ajili ya watu wa kizazi hiki kama walivyofanya Warosmini waliowatangulia
katika maisha ya kitawa.
Watawa wanahimizwa kumwilisha ndani mwao, Heri za
Mlimani, ambazo kimsingi ni muhtasari wa Mafundisho Makuu ya Yesu kwa wafuasi wake;
tayari kuwaendea maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii ili kuwatangazia
Injili ya Furaha na kuwaonjesha huruma na upendo wa Mungu, kama anavyokazia Baba Mtakatifu
Francisko. Watawa wanahamasishwa na Mama Kanisa kama walivyo waamini wengine wote
kujitahidi kuwa watakatifu, kwa kumfuasa Kristo aliyekuwa: Mtii, Mseja na Fukara.
Kristo awe ni utambulisho wa maisha na sadaka yao ya kitawa.
Yesu ni kielelezo
cha sura ya Mungu katika maisha ya mwanadamu anasema Padre Nardin katika mahubiri
yake ya kwanza katika tukio kama hili tangu alipochaguliwa hivi karibuni kuliongoza
Shirika la Mapendo. Watawa wanakumbushwa kwamba, maisha ya kitawa ni mwaliko wa kujisadakisha
kwa ajili ya Mungu, Kanisa na Jirani. Maisha haya yawe ni mwanga unaoleta matumaini
mapya mintarafu mapenzi ya Mungu kwa watu wake.
Watawa walioweka Nadhiri za
daima, wametakiwa kuwa ni wachapakazi, wanyenyekevu, wavumilivu kwani katika hija
ya maisha na utume wao, watakumbana na vikwazo pamoja na vizingiti, lakini hawapaswi
kukata tamaa, bali wasonge mbele kwa kutambua kwamba, Mwenyezi Mungu amewaita na atawategemeza
katika maisha na utume wao.
Wasikatishwe tamaa na mapungufu ya kibinadamu
yanayofanywa na baadhi ya viongozi wa Shirika au Kanisa; wasaidiane kidugu, huku wakiheshimiana
na kwamba, wanapaswa kujisikia kuwa ni sehemu ya Jumuiya inayojengeka katika msingi
wa mapendo ya kidugu! Ushuhuda wa umoja na mshikamano, kiwe ni kikolezo, mvuto na
mashiko kwa wale wanaowazunguka, katika kumfuasa Yesu Kristo.
Padre Vito Nardon
amewaweka wanashirika wapya chini ya ulinzi na usimamizi wa Bikira Maria wa miito,
ili awasaidie kujifunza: haki, upendo na kuyasadakisha maisha yao kwa ajili ya Mungu
na jirani. Watawa walioweka nadhiri zao za daima ni: Aji Alphonce kutoka India, Aristid
Shayo kutoka Tanzania na Justus Okibo kutoka Kenya.