2013-12-10 11:08:26

Tata Madiba, kweli alikuwa ni mtu wa watu!


Tangu Mzee Nelson Mandela alipofariki dunia tarehe 5 Desemba 2013, nyumbani kwake, kuliwekwa hema kwa ajili ya sala, tafakari na rambi rambi. Viongozi mbali mbali kutoka katika Jumuiya ya Kimataifa wamekuwa wakikusanyika kwenye hema hili ili kutoa salam zao za rambi rambi kwa Familia ya Mzee Madiba, mtu aliyejitoa bila ya kujibakiza kwa ajili ya kutetea misingi ya haki, amani, usawa na maendeleo endelevu kwa wananchi wote wa Afrika ya Kusini.

Kati ya viongozi kutoka Jumuiya ya Kimataifa waliofika kusali na kutafakari pamoja na Familia ya Mzee Madiba ni Dr. Olav Fyske Tveit, Katibu mkuu wa Baraza la Makanisa Ulimwenguni aliyeihakikishia Familia ya Mzee Mandela uwepo wa karibu kwa njia ya sala kutoka kwa Makanisa 345 kutoka sehemu mbali mbali za dunia. Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Bwana Ban Ki-Moon na Askofu mkuu mstaafu Demond Tutu ni kati ya viongozi waliohudhuria tukio hili, kabla ya mamillioni ya watu kushiriki kutoka heshima zao za mwisho, kwenye Uwanja wa michezo wa Afrika ya Kusini, Jumanne, tarehe 10 Desemba, 2013.

Habari zinasema kwamba, zaidi ya viongozi wakuu wa nchi walioko madarakani na wastaafu wanahudhuria kwenye tukio hili la kihistoria, dunia inaposimama kuomboleza kifo cha Mzee Madiba. Hii ni changamoto anasema Dr. Tveit kwa watu wa nyakati hizi kwamba, haki, amani na msamaha vinaweza kutawala katika mioyo ya watu, ikiwa kama watapania kufanya hivi! Amani inapatikana kwa njia ya haki; mambo yanayoweza kubadili sura ya dunia na kuifanya kuwa ni mahali pazuri zaidi pa kuishi.

Tangu asubuhi na mapema, wananchi wengi nchini Afrika ya Kusini wamekuwa wakifurika mjini Johannesburg ili kutoa heshima zao za mwisho, licha ya mvua kubwa iliyokuwa inaendelea kunyeesha! Maziko ya Tata Madiba yamekuwa ni kielelezo cha upatanisho wa kimataifa. Mwanasiasa mkongwe kutoka Afrika, aliyeishi kizuizini kwa miaka 27, lakini alipotoka gerezani hakuwa na chembe hata kidogo ya dhana ya kutaka kulipiza kisasi.







All the contents on this site are copyrighted ©.