2013-12-10 09:38:35

Papa azindua kampeini ya kufuta njaa duniani


Kupitia ujumbe kwa njia ya video, Papa Francisko ametoa wito kwa watu wote duniani, kuunga mkono kampeni mpya ya Shirika la Caritas Internationalis, inayolenga kufuta njaa duniani.Shirika la Caritas Internationalis, ni mkono wa Kanisa Katoliki katika utoaji wa misaada ya ubindamu, na hushirikiana na mashirika mengine wabia yapatayo 164, na hufanya kazi katika mataifa 200 duniani kote.

Papa Francisko katika ujumbe huo wa Jumatatu jioni, alitaja kazi za Caritas, ziko ndani ya moyo wa utume wa Kanisa, na hasa katika nia yake kuwa karibu na wale wote wanaokabiliwa na maafa kama njaa, watu wenye njaa, ambao hata Bwana alitambua dhiki yao na kusema,” nilikuwa na njaa nanyi mkanilisha."

Aidha katika ujumbe wake, Papa amekumbusha wakati Mitume walipo mwambia Yesu kwamba, watu waliokuja kumsikiliza wana njaa, nae akawambia nendeni mkawatafutie chakula. Wao wenyewe mitume hawakuwa na kitu , walikuwa mikate mitano na samaki wawili tu. Lakini kwa neema ya Mungu , waliweza kulisha umati wa watu , hata kusimamia na kukusanya kile kilicho baki , wakiepusha kisiharibike na kutupwa kama taka.


Papa anasema, hata Sisi leo hii, tupo mbele ya kashfa ya kimataifa ya karibu watu bilioni moja , wanakabiliwa na njaa leo. Hatuwezi kujifanya kama vile hatutambui hilo na kutazama kwingine.Hiyo ni hali halisi, watu wana njaa, ingawa dunia ina chakula cha kutosha kulisha kila mtu. Hivyo mfano wa kuzidisha mikate mitano na samaki wawili ni fundisho kwetu kwamba, tukiwa na nia , tulicho nacho kamwe hakiwezi kutuishia. Daima kibaba kitajaa tele na hakuna kitakacho potea bure.

Kwa mtazamo huo, Papa alitoa mwaliko kila mtu , kutengeneza nafasi katika moyo wake kwa ajili ya dharura hii ya kuheshimu haki iliyotolewa na Mungu mwenyewe kwa kila mtu ya kupata chakula cha kutosha . Tunapashwa kushirikishana kwa upendo wa kikristo na wale ambao wanakabiliwa na vikwazo mbalimbali, katika kukidhi mahitaji ya msingi , kama chakula. Na wakati huo huo , Kukuza ushirikiano halisi na watu Maskini, ili kupitia matunda ya kazi zao na kazi zetu , wanaweza kuishi maisha ya heshima.

Kwa maneno hayo , Papa aliendelea kuzitaka taasisi zote duniani , kanisa na , kila mmoja, kutenda kama familia moja ya binadamu, katika kutoa sauti kwa niaba ya wale wote ambao wanakabiliwa na mateso ya kimyakimya yanayotokana na njaa, ili sauti hiyo, iweze kupata kishindo cha kuitingisha dunia, katika kuiona haja ya kukomesha njaa .

Aidha Papa amesema, kampeini hii, pia ni mwaliko kwetu sote , unao tutaka tuwe waangalifu zaidi katika uchaguzi wa chakula, ambao mara nyingi husababisha chakula kupotea na uwepo wa matumizi mabaya ya rasilimali tulizo nazo. Pia ni tunakumbushwa kuacha kufikiria kwamba , utendaji wetu wa kila siku , hauna athari kwa maisha ya wale ambao wanakabiliwa na njaa.

Mwisho wa Ujumbe wake, Papa aliahidi ushirikiano wake wa dhati kwa mashirika ya misaada ya Caritas, katika kampeni hii, ambamo yatatenda kama familia moja ya binadamu kwa ajili ya kutafuta chakula kwa wote.
Papa ameomba kwamba Bwana, aijalie dunia neema zake ili , pasiwe tena na mtu anayekufa kwa njaa. Pamoja na ombi hilo, Papa pia alitoa baraka zake kwa wote.










All the contents on this site are copyrighted ©.