Njia mpya za mawasiliano ya kijamii zinaendelea kuleta mabadiliko na changamoto kubwa
katika Jamii. Barani Ulaya, mitandao ya kijamii imekuwa ni jukwaa maalum kwa ajili
ya majiundo ya binadamu, mahali ambapo watu wanawasiliana na kushirikishana mang’amuzi
ya maisha sanjari na ujenzi wa mahusiano ya kijamii, hasa miongoni mwa vijana wa kizazi
kipya.
Ni jukwaa
linalogusa undani wa maisha ya mwanadamu kwa kutumia lugha, mbinu mpya na zile za
zamani katika kufikisha ujumbe kwa hadhira inayokusudiwa.
Hii ni fursa makini
inayolihamasisha Kanisa kuhakikisha kwamba, linapeleka ujumbe wa Injili unaogusa sakafu
za mioyo ya watu! Uinjilishaji mpya ni dhamana inayotekelezeka hata kwa njia ya sana
na kwamba, kuna uhusiano wa karibu sana kati ya Liturujia na Uhandisi. Mababa wa Mtaguso
mkuu wa Pili wa Vatican wamekuwa wakilihamasisha Kanisa kusoma alama za nyakati pamoja
na kuhakikisha kwamba, linatumia maendeleo ya sayansi na teknolojia ya habari katika
azma ya Uinjilishaji Mpya.
Baba Mtakatifu Francisko ameendelea kuonesha umuhimu
wa matumizi ya mitandao ya kijamii katika mchakato wa Uinjilishaji Mpya. Hadi sasa
anazaidi ya wafuasi millioni kumi katika akaunti yake ya twitter. Hii inaonesha kwamba,
Kanisa linaweza kujikita katika Uinjilishaji Mpya hata kwa kutumia mitandao ya kijamii.
Mama Kanisa anapofanya kumbu kumbu ya Miaka 50 tangu Hati ya Kichungaji kuhusu Vyombo
vya Mawasiliano ya Kijamii, Inter Mirifica ilipotolewa kwa mara ya kwanza na Mababa
wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican, Kanisa bado lina changamotishwa kusoma alama za
nyakati sanjari na matumizi sahihi ya vyombo hivi kwa kuzingatia: sheria, kanuni,
utu na maadili mema.
Haya ni kati ya mambo msingi yaliyojadiliwa na wajumbe
Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Ulaya, katika mkutano wa Maaskofu wenye
dhamana ya vyombo vya habari kutoka katika Mabaraza husika. Mkutano huu uliofanyika
mjini Barcelona, umeongozwa na kauli mbiu “uinjilishaji wa roho za waamini Barani
Ulaya”. Wajumbe wamepembua changamoto zinazolikabili Kanisa katika utekelezaji wa
dhamana yake ya Umissionari; mchakato wa mawasiliano unaofanywa na Baba Mtakatifu
Francisko, kiasi cha kuwagusa watu wengi pamoja na teknolojia mpya za mawasiliano
ya kijamii.
Waamini wanaalikwa kwa namna ya pekee kuona ukuu na matendo ya
Mungu kwa njia ya sanaa ya uhandisi, jambo linaloonesha ushuhuda wa mwamini aliyefanya
tafakari ya kina kwa kukutana na Yesu, kama anavyokazia Baba Mtakatifu Francisko.
Matumizi ya njia mpya za mawasiliano ni kati ya mambo yaliyosababisha mabadiliko makubwa
katika maisha na utume wa Majimbo kadhaa Barani Ulaya, kama ilivyo jidhihirisha katika
Jimbo kuu la Barcelona. Mambo yote haya yamejadiliwa kwa kina ili kulisaidia Kanisa
kutoa majibu makini katika kukabiliana na changamoto hizi.
Askofu mkuu Claudio
Maria Celli, Rais wa Baraza la Kipapa la Mawasiliano ya Jamii anasema, Mababa wa Mtaguso
mkuu wa Pili wa Vatican walikazia kwa namna ya pekee usomaji wa alama za nyakati kwa
kuendelea kutumia njia za mawasiliano ya Kijamii kwa ajili ya Uinjilishaji. Wakati
huu Mama Kanisa hana budi kujikita pia katika matumizi ya mitandao ya kijamii ili
kuhakikisha kwamba, ujumbe wa Habari Njema ya Wokovu unawafikia watu mahali walipo!
Anasema,
Mama Kanisa hakutumwa kuinjilisha mitandao, bali kuinjilisha kwa njia ya mitandao,
yaani kuwatangazia watu wanaoishi katika ulimwengu wa utandawazi na maendeleo ya sayansi
na teknolojia kwa kutumia lugha na nyenzo bora ili kuwafikia watu wengi zaidi. Huu
ni ujumbe unaopaswa kumwilishwa kwa njia ya maneno yanayojidhihirisha katika matendo,
kwa maneno mengine, hii ndiyo imani tendaji.
Mitandao ya kijamii ikitumiwa
vyema inaweza kusaidia kuhamasisha kundi kubwa la watu, ili kuwa na mwelekeo na sera
makini zaidi zinazozingatia ut una heshima ya binadamu. Mitandao ya kijamii imetumika
nchini Ufaransa kuhamasisha waamini na watu wenye mapenzi mema, kusimama kidete kupinga
ndoa za watu wa jinsia moja kwani zinakwenda kinyume cha mapenzi ya Mungu na utu wema.
Mafanikio makubwa yamejionesha kwa namna ya pekee nchini Ufaransa.
Kanisa halina
budi kutumia njia za mawasiliano kadiri ya mapokeo pamoja na njia za kisasa, ili kuwagusa
watu wengi zaidi, kadiri ya mahitaji ya hadhira inayokusudiwa. Baba Mtakatifu katika
uongozi wake tangu alipochaguliwa ameonesha jinsi ya kuwasiliana katika uhalisia wa
maisha pasi na “mkwara” na kwamba, ujumbe wa Kikristo unaosimikwa katika mapendo kwa
Mungu na jirani, unaendelea kuwagusa watu wengi zaidi.
Baba Mtakatifu anafundisha
Injili ambayo ameifanyia tafakari ya kina na anapenda kuimwilisha kwa njia ya matendo.
Ni kiongozi anayependa kuzungumza na mtu mmoja mmoja na wala si makundi ya watu! Anapenda
kumwita mtu kwa jina! Mwishoni, wajumbe wameshauri kwamba, Maaskofu wenye dhamana
ya kusimamia vyombo vya upashanaji habari wanapaswa kukutana mara kwa mara, ili kuimarishana
na kubadilishana uzoefu na mang’amuzi tayari kupambana na changamoto zinazojitokeza
katika ulimwengu wa mawasiliano ya kijamii.