2013-12-10 08:58:29

Guinea Bissau: kufunga na kusali hapo tarehe 13 Desemba 2013 ili kuombea Amani Duniani


Baraza la Maaskofu Katoliki Guinea Bissau linawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema kufunga na kusali hapo tarehe 13 Desemba 2013 kwa ajili ya kuombea amani duniani, Barani Afrika na kwa namna ya pekee nchini Guinea Bissau.

Maaskofu wanapenda kumwomba Mwenyezi Mungu kwa njia ya sala, maombi na mfungo ili aweze kuwakirimia ujasiri kwa kupokea zawadi ya amani kwa njia ya ushuhuda wa maisha yanayosimikwa katika: ukweli, haki na upatanisho. Viongozi wa Jumuiya ya Kimataifa, viongozi kutoka Barani Afrika na viongozi wa Guinea Bissau hawana budi kusimama kidete kulinda na kutetea maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii.

Wananchi wanapaswa kujikita katika ari na moyo wa kutetea demokrasia ya kweli, utu wema, kanuni na maadili ya kazi. Viongozi, wanasiasa na wanajeshi ambao wanadhamana ya kulinda mafao ya wengi wawe na ujasiri wa kuonesha tunu hizi msingi katika maisha na vipaumbele vyao. Jamii zijenge na kuimarisha mshikamano wa kimataifa.

Maaskofu wanawaalika wananchi wa Guinea Bissau hata katika umaskini wao, kile kidogo watakachojinyima, wakikusanye kwa ajili ya kuwasaidia wananchi wa Ufilippini, waliokumbwa na tufani, iliyosababisha maafa makubwa kwa watu na mali zao. Kwa kuguswa na mahangaiko ya wananchi wa Ufilippini, Baraza la Maaskofu Katoliki Guinea Bissau limeamua kwamba, Jumapili ya Nne ya Kipindi cha Majilio, yaani hapo tarehe 22 Desemba, 2013, waamini watakusanya sadaka kwa ajili ya kuwasaidia wananchi wa Ufilippini.

Maaskofu wa Guinea Bissau pamoja na waamini hivi karibuni wameadhimisha Siku kuu ya Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili kwa hija na maandamano makubwa katika Madhabahu ya Bikira Maria wa Cacheu, wakiongozwa na kauli mbiu "Pamoja na Bikira Maria tunatembea katika Mwanga wa Imani. Hija hii imehudhuriwa na waamini wa dini na madhehebu mbali mbali ya Kikristo kama kielelezo cha mshikamano wa dhati katika kuombea: haki, amani na upatanisho wa kweli miongoni mwa Jamii.







All the contents on this site are copyrighted ©.