2013-12-10 09:12:44

Baada ya mauaji ya kinyama, hali ya utulivu inaanza kurejea tena mjini Bangui!


Hali ya amani na utulivu inaanza kurejea tena mjini Bangui, Jamhuri ya Watu wa Afrika ya Kati, ingawa bado kuna idadi kubwa ya watu wasiokuwa na makazi maalum wanaendelea kuishi katika Parokia baada ya kutokea mapigano kati ya Jeshi la Seleka na kikundi cha Balaka na hivyo kusababisha maafa makubwa. Hali ya utulivu imerejea tena baada ya wanajeshi 1,600 kutoka Ufaransa kuwasili mjini Bangui.

Maisha ya kawaida yanaanza kurudia tena, viwanja vya ndege vimefunguliwa na magari ya abiria yanafanya kazi kama kawaida. Askofu Juan Jose Aguirre Munos wa Jimbo Katoliki la Bangassou anasema watu bado wana wasi wasi kuhusu usalama wa maisha na mali yao kwani bado kuna mauaji ya kinyama yanayoendelea kufanywa na wanajeshi wa Seleka. Itakumbukwa kwamba, hivi karibuni zaidi ya watu 400 walipoteza maisha mjini Bangui.

Jeshi la kulinda amani kutoka katika Umoja wa Afrika, wanaendelea pia kusaidia kulinda na kudumisha amani mjini Bangui. Askofu Juan Jose Aguirre Munos anasema, viongozi wa kidini wanaendelea kuhamasisha wananchi kujenga utamaduni wa kuvumiliana, kuheshimiana na kuthaminiana na kamwe tofauti zao za kidini kisiwe ni chanzo cha kuwatumbukiza watu katika majanga ya maisha!







All the contents on this site are copyrighted ©.