2013-12-09 08:47:22

Papa atoa heshima zake kwa Sanamu ya Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili.


Baba Mtakatifu Francisko, akifuata desturi zilizowekwa na watangulizi wake, Jumapili, katika kuiadhimisha Siku Kuu ya Bikira Maria Mkingiwa dhambi ya Asili, alitoa heshima zake kwa sanamu ya Mama Maria, inayoheshimiwa sana na Wakazi wa Roma, iliyoko katika uwanja wa Spagna, ambako alihitimisha Siku kuu hii kwa sala na maombi kama pia ilivyo fanywa na Mapapa wengine waliomtangulia.

Sehemu hiyo, Ibada ya sala na maombi ilianza na somo kutoka kitabu cha Ufunuo, ambamo Maria anaelezwa kuwa mwanamke, aliyevikwa jua, na mwezi chini ya miguu yake , na kichwani mwake akiwa na taji la nyota kumi na mbili " (Ufu. 12:01 ) .
Kisha Baba Mtakatifu, alitoa sala kwa Mama Maria mkingiwa dhambi ya asili, akiomba msaada wa Mama, ili waamini wa mwanae, waweza kuamsha ndani mwao, hamu mpya kwa ajili ya maisha Matakatifu, yenye kuuwasilisha na kushuhudia uzuri wote wa Injili katika maisha ya kila siku.

Aliendelea kuomba msaada wa maombezi yake, yatusaidie kubaki makini katika kuisikia sauti ya Bwana , na kamwe kutokuwa tofauti na kilio cha maskini, wagonjwa, wazee, watoto, na kila maisha ya binadamu. Papa kabla ya kuondoka katika uwanja huo, alimsalimu wagonjwa na walemavu waliokuwa wamekusanyika katika uwanja huo kwa ajili ya maadhimisho.

Baada ya maadhimisho hayo, Papa Francis alifanya ziara fupi katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Maria Mkuu ambako alitolewa maombi yake faraghani mbele ya sanamu Mama Yetu “Salus Populi Romani “

Sanamu ya Mama Yetu asiyekuwa na Ndoa, katika Uwanja wa Spagna, iliwekwa wakfu Desemba 8, 1857, ikiwa imepita miaka kadhaa tangu kupitishwa kwa mafundisho sadikifu ya kanisa kwamba Maria alikingiwa dhambi ya asili tangu alipotungwa mimba. Na umekuwa ni utamaduni kwa Papa kutoa heshima kwa sanamu hizi za Bikira Maria Mkingiwa dhambi ya Asili , kila mwaka Desemba 8 kama sehemu ya maadhimisho ya sikukuu Maria Mkingiwa dhambi ya Asili.








All the contents on this site are copyrighted ©.