2013-12-09 09:00:14

Neno la Mungu liwaandae waamini kumpokea Kristo Masiha!


Baraza la Maaskofu Katoliki Uingereza na Wales, limetumia Jumapili ya Pili ya Kipindi cha Majilio kwa ajili ya kuhamasisha: kusoma, kutafakari na kumwilisha Neno la Mungu katika maisha ya waamini, hasa wakati huu Mama Kanisa anapojikita katika azma ya uinjilishaji mpya.

Hii ni sehemu ya mchakato wa maandalizi ya Maadhimisho ya Siku kuu ya Noeli, Kristo anapozaliwa tena katika maisha ya watu wake. Waamini wanahamasishwa kuhakikisha kwamba, wanajifunza Neno la Mungu kama njia ya kukutana na Yesu, ili aweze kuwaonjesha ile Injili ya Furaha wanayotumwa kuwatangazia jirani zao, ili kuwajengea moyo wa imani na matumaini hasa wakati huu wanapokabiliana na majanga ya maisha!

Maaskofu wanawahamasisha waamini katika Salam zao za Noel ina zawadi kwa wapendwa wao, wahakikishe kwamba, walau wanatumia sehemu ya Neno la Mungu kama matashi mema. Kipindi cha Majilio na hatimaye Noeli, ni wakati wa pilika pilika nyingi za maisha, hali inayoweza kuwafanya baadhi ya watu kupata msongo wa mawazo na mahangaiko ya ndani.

Kumbe, Neno la Mungu liwe ni chemchemi ya matumaini na faraja kwa wote. Waamini wajenge mahusiano mema ya kijamii, kwani Kristo anayezaliwa kati yao, ni Neno aliyefanyika mwili katika mambo yote akawa sawa na binadamu isipokuwa Yeye hakutenda dhambi. Neno la Mungu liwawezeshe waamini kutambua maana ya Majilio na Siku kuu ya Noeli katika maisha na vipaumbele vyao.

Kipindi cha Majilio ni wakati wa kuonjeshana upendo wa dhati kwa maisha ya kawaida, badala ya kujitumbukiza katika anasa na kupenda mno starehe. Ni wakati wa toba na wongofu wa ndani, ili kurekebisha mahusiano kati ya mtu na jirani yake na kati ya mtu na Muumba wake. Kipindi cha Majilio, kiwe kweli ni fursa ya kujiandaa kukutana na Yesu Kristo Mkombozi wa dunia, kwa njia ya Tafakari ya Neno la Mungu, Matendo ya huruma na maisha adili.








All the contents on this site are copyrighted ©.