2013-12-09 09:18:00

Kanisa la Waadventisti lazindua Jimbo kuu Kusini mwa Tanzania


Waziri mkuu wa Tanzania Mizengo Pinda amewataka Watanzania waendelee kuombea amani, ustawi na maendeleo ya Taifa zima bila kujali tofauti zao za dini na kusisitiza kwamba kila mmoja ana wajibu wa kutunza amani iliyopo.
Ametoa wito huo Jumamosi, Desemba 7, 2013 wakati akizindua Jimbo Kuu la Kusini mwa Tanzania (Southern Tanzania Union Mission) la Kanisa la Waadventista Wasabato kwenye sherehe zilizofanyika kwenye Viwanja vya Mwalimu J. K. Nyerere, barabara ya Kilwa jijini Dar es Salaam.
Akizungumza na waumini zaidi ya 13,000 wa Kanisa hilo walioshiriki uzinduzi huo, Waziri Mkuu alisema: “Mtu asiyejua vurugu hawezi kujua thamani ya amani... lakini lazima tujue madhara ya vurugu huwa ni makubwa kwa watoto, wanawake na wazee.” Aliwasihi viongozi wa kanisa hilo pamoja na waumini kuendelea kuliombea Taifa pamoja na Watanzania wote. “Mimi huwa nafarijika sana ninaposikia sehemu fulani kuna maombi kwa ajili ya Taifa, kwa hiyo ninawaomba Maaskofu na waumini msichoke kuliombea Taifa letu,” alisema.
Mbali na kuliombea Taifa pamoja na kuwaombea waamini wake, Waziri Mkuu aliwataka viongozi wa Kanisa kuendelea kushirikiana na Serikali kutafuta njia ya kuwasaidia waamini wake kukua kiuchumi. “Kanisa lina wajibu wa kuwasaidia wananchi kukua kiuchumi na mimi natambua waamini wa Kanisa hili ni wakulima na wafugaji ama vyote viwili.”
Waziri Mkuu alisema moja ya kazi kubwa ya kanisa ni kusaidia waumini wake kukua kiroho na kimwili. Lakini kanisa pia linahitaji kuona maisha ya waumini yanakuwa bora zaidi. ”Tunategemea uchumi wa muumini mmoja mmoja kukua na hivyo uchumi wa kanisa, na uchumi wa Taifa kwa ujumla kukua,” aliongeza.
Alisema anataraji kwamba kupatikana kwa Jimbo Kuu la Kusini kutakuwa ni chachu ya kupata maendeleo zaidi ya kiuchumi katika Jimbo hilo ambalo linafaa sana kwa kilimo. “Pia, tunategemea kasi ya kupata waumini wapya itaongezeka kutokana na kugawanywa kwa Jimbo Kuu moja na kuwa Majimbo Makuu mawili, hivyo kusogeza huduma za kiroho na kiuchumi karibu zaidi na waamini,” alisema.
Waziri Mkuu alisema Jimbo Kuu la Kusini lililozinduliwa jana linajumuisha mikoa ambayo ni maarufu kwa shughuli za kiuchumi. “Imetajwa mikoa takriban 11 ya Tanzania Bara na Mitano ya Visiwani. Ipo mikoa ya Dar es Salaam, Dodoma, Iringa, Katavi, Lindi na Mbeya. Mikoa mingine ni Morogoro, Mtwara, Pwani, Rukwa na Ruvuma. Hakika ni eneo kubwa la kuongoza.”
“Kinachotakiwa ni kwa Kanisa kujipanga vizuri kwa kujiwekea mikakati ya maendeleo. Nawaombeni sana kuanzia sasa, tuwahimize waumini wetu hasa vijana wajikite pia katika kuanzisha miradi ya kilimo na ufugaji, ikiwemo kilimo cha mazao na ufugaji nyuki. Mkitumia fursa hizi zinazowazunguka katika maeneo yetu ya Jimbo hili, mnaweza kabisa kuleta ukombozi wa kiuchumi, hususan kwa vijana wetu,” alisisitiza.

Kanisa hilo lenye waumini wapatao milioni 17.2 duniani, lina makao yake makuu nchini Marekani. Hapa Tanzania lina waumini milioni tano na lilikuwa na jimbo kuu moja ambalo liligawanywa katika majimbo sita na makao yake makuu kwenye mabano kama ifuatavyo:- Kaskazini Mashariki (Same), Kusini mwa Ziwa Victoria (Mwanza), Mara (Musoma), Mashariki (Morogoro), Nyanda za Juu Kusini (Mbeya) na Magharibi (Kigoma).
Mapema, akisoma risala mbele ya Waziri Mkuu, Katibu Mkuu wa Jimbo Kuu la Kusini, Mchungaji James Machage alisema kutokana na kupanuka kwa kazi, kanisa hilo limeona vema hapa nchini kuwe na majimbo makuu mawili badala ya moja. Alisema Jimbo Kuu la Kaskazini ambalo makao yake makuu yatakuwa Arusha litahusisha majimbo ya Mara, Kusini mwa Ziwa Victoria, Magharibi na Kaskazini Mashariki wakati Jimbo Kuu la Kusini litahusisha majimbo ya Mashariki na Nyanda za Juu Kusini na makao yake makuu yatakuwa Jijini Dar es Salaam.








All the contents on this site are copyrighted ©.