Afrika ya Kusini, Jumapili iliyopita imetumia siku hii kwa ajili ya kusali, kufunga
na kutafakari kuhusu mchango wa Mzee Nelson Mandela, enzi ya uhai wake. Wananchi wa
dini na madhehebu mbali mbali wameungana kusali ili kumwombea Tata Madiba pamoja na
kuliombea Taifa la Afrika ya Kusini, linapoanza awamu mpya baada ya kifo cha Mzee
Madiba.
Rais Jacob Zuma anasema, Mzee Madiba alijipambua kwa tunu msingi za
maisha ya kiutu, ni kama mwanga uliotumwa kufukuza giza na vivuli vilivyokuwa vinamsonga
mwanadamu. Aliwapatia watu wake matumaini makubwa na akawatengenezea maisha kwa leo
na kesho iliyo bora zaidi. Alionesha moyo wa kusamehe na kusahau; alikuwa ni mtu wa
haki na ukarimu kwa jirani zake; alisimama kidete kulinda na kutetea zawadi ya uhai.
Bwana
Josè Graziano da Silva, Mkurugenzi mkuu wa Shirika la Kilimo na Chakula la Umoja wa
Mataifa, FAO anamkumbuka Mzee Mandela, kwa kusimama kidete dhibi ya baa la njaa na
umaskini duniani, kama kielelezo cha uhuru wa kweli kwa binadamu. Akawataka wakuu
wa Jumuiya ya Kimataifa kutunga sera makini katika mapambano dhidi ya baa la njaa
na umaskini. Hata leo hii kuna watu millioni 842 ambao wanakabiliwa na baa la njaa
duniani.
Shirika la Wakimbizi la Umoja wa Mataifa linasema kwamba, Mzee Madiba
alionesha ushirikiano wa hali ya juu katika kukabiliana na tatizo la wakimbizi duniani.
Aliguswa na hali ya wakimbizi kutoka Afrika ya Kusini, waliokuwa wamelazimika kuikimbia
nchi yao kutokana na utawala wa ubaguzi wa rangi Afrika ya Kusini, enzi hizo.
Ni
kielelezo cha mwanasiama mahiri aliyetambua na kuonja shida za wahamiaji, ambao hata
leo hii wanalazimika kuzikimbia nchi zao kutokana na vita, kinzani, majanga asilia
pamoja na kutafuta fursa za ajira.
Bwana Anthony Lake, Mkurugenzi mkuu wa Shirika
la kuhudumia Watoto la Umoja wa Mataifa, UNICEF anasema kwamba, tangu mwaka 2002 Mzee
Madiba alijitoa mhanga kwa ajili ya kampeni ya kuwasaidia watoto kupata haki yao msingi
ya elimu. Watoto millioni mbili kutoka Barani Afrika wakabahatika kupata fursa ya
kwenda shule. Alishirikiana kwa karibu sana na UNICEF ili kuhakikisha kwamba, elimu
kwa watoto wadogo inakuwa ni sehemu ya ajenda za maendeleo kwa Jumuiya ya Kimataifa.