Barua ya kichungaji kutoka kwa Baraza la Maaskofu Katoliki Zimbabwe
Baraza la Maaskofu Katoliki Zimbabwe katika barua yake ya kichungaji iliyotolewa hivi
karibuni linasema, nchi ya Zimbabwe inakwenda mrama kuliko hata ilivyokuwa kabla ya
uchaguzi mkuu, uliompatia ushindi wa kishindo Rais Robert Mugabe wa Zimbabwe. Hali
ya maisha ya wananchi wengi inaendelea kudorora, kiasi cha kuweka rehani tunu msingi
za haki, amani na usalama wa raia.
Wananchi wa Zimbabwe wanaendelea kukata
tamaa kutokana na ukata wa maisha na hakuna juhudi za makusudi zinazofanywa na Serikali
iliyoko madarakani ili kurekebisha hali hii. Huduma za elimu, afya, maji safi na salama
pamoja na miundo mbinu ni mambo ambayo yanapaswa kushughulikiwa kwa haraka kwani hali
ni mbaya, kuliko inayodhaniwa na wengi! Mgawo wa maji na umeme umekuwa ni wimbo wa
kawaida kwa wananchi wa Zimbabwe, hali ambayo inakwamisha maendeleo endelevu na jitihada
za wananchi kujikwamua kutoka kwenye umaskini wa hali na kipato.
Baraza la
Maaskofu Katoliki Zimbabwe katika barua yake ya kichungaji linasema kwamba, kuna haja
kwa Serikali na wadau mbali mbali wa maendeleo kuwa na sera na mbinu mkakati utakaorekebisha
huduma katika sekta ya elimu, afya, maji, nishati na usafirishaji. Zimbabwe ianze
tena mchakato wa ujenzi wa uhusiano wa kimataifa, ili kusaidia marekebisho ya kiuchumi,
kwa kuwa na soko lenye uhakika pamoja na kuirudishia Zimbabwe hadhi yake ya kuwa ni
mzalishaji mkuu wa mazao ya chakula na biashara kusini mwa Afrika, ili kuwa na uhakika
wa usalama wa chakula kwa watu wengi Zaidi!
Maaskofu Katoliki Zimbabwe wanasema,
viwanda vimebaki kuwa ni magofu na maficho ya makundi ya wahuni na majambazi. Utu
na heshima ya wananchi wa Zimbabwe inashushwa kwa kuuziwa bidhaa hafifu zisizo na
ubora wala viwango. Uchaguzi mkuu wa Mwezi Julai, 2013, uliohitimisha Serikali ya
Umoja wa Kitaifa iliyokuwa imeundwa baada ya kinzani za uchaguzi mkuu wa Mwaka 2008,
haujaonesha matumaini waliyokuwa nayo wananchi wa Zimbabwe.
Umaskini wa hali
na kipato umeongezeka, wananchi wengi wanalazimika kwenda kuhemea katika nchi za jirani
hata kwa mambo ya kawaida kabisa! Ushirikiano kati ya vyama vya kisiasa kwa ajili
ya mafao ya wengi, unaonekana kutoweka kabisa! Maaskofu wanawahamasisha wanasiasa
nchini Zimbabwe kushirikiana kwa karibu zaidi kwa ajili ya kutetea: haki msingi za
binadamu, ustawi, maendeleo na mafao ya wengi!
Zimbabwe ni kati ya nchi chache
za Kiafrika zilizobahatika kuwa na utajiri mkubwa wa rasilimali na mali asili; Watu
wanaomcha Mungu; wenye ujuzi na maarifa; mambo yote haya yakitumiwa vyema yanaweza
kuleta mwamko mpya wa maendeleo na ubora wa maisha kwa wananchi wengi wa Zimbabwe.
Kuna haja kwa wanasiasa kuwa na utashi wa kisiasa, ili kusimama kidete kulinda
na kutetea mafao ya wengi. Maaskofu wanawaalika wadau mbali mbali kujifunga kibwebwe
ili kushirikiana na kushikamana kwa pamoja kwa ajili ya kutunga sera na mikakati ya
maendeleo katika sekta mbali mbali za maisha ya wananchi wa Zimbabwe na utengemanano
wa Kikanda na katika Jumuiya ya Kimataifa.