Uwepo wa Kanisa katika mitandao ya kijamii ni kuwaonjesha watu huruma ya Mungu inayofunuliwa
kwa njia ya Neno wa Mungu aliyefanyika mwili!
Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican umewapatia nafasi waamini walei kuweza kuchangia katika
ustawi, maisha na utume wa Kanisa kwa kutambua kwamba, wanatumwa ulimwenguni ili kuweza
kuyatakatifuza malimwengu.
Hizi ndizo juhudi zilizofanywa na Baraza la Kipapa
kwa ajili ya Walei katika Maadhimisho ya Kongamano la Waamini Walei Barani Afrika
lililofanyika kunako Mwaka 2012; nafasi ya wanawake, kama sehemu ya Maadhimisho ya
Jubilee ya Miaka 25 tangu Mwenyeheri Yohane Paulo II alipochapisha Waraka juu ya Heshima
ya Wanawake, Mulieris Dignitatem. Katika ulimwengu wa utandawazi, wanawake wanapaswa
kua mstari wa mbele katika kumlinda mwanadamu.
Kanisa limeendelea pia kuwekeza
katika majiundo makini kwa vijana, katika Maadhimisho ya Siku za Vijana Duniani kama
ilivyotokea mjini Rio de Janeiro, Brazil. Vijana wamehamsishwa kuendeleza asili na
dhamana ya Kanisa ambalo kimsingi ni la Kimissionari, ili kutangaza Injili ya Furaha
kwa watu wa mataifa, baada ya kukutana na Yesu Kristo katika hija ya maisha yao ya
kiroho, ili waweze kuleta mabadiliko na matumaini ya maisha kwa jirani zao!
Ni
maneno ya Baba Mtakatifu Francisko, wakati alipokutana na kuzungumza na Wajumbe wa
Baraza la Kipapa kwa ajili ya Walei, waliokuwa na mkutano wao wa Mwaka kuanzia tarehe
5 hadi tarehe 7 Desemba 2013, kwa kuongozwa na tema "Kumtangaza Kristo nyakati za
Dijitali".
Mitandao ya kijamii anasema Baba Mtakatifu ni jukwaa muhimu sana
la Uinjilishaji miongoni mwa vijana. Maendeleo ya mitandao ya kijamii yanahitaji kwa
namna ya pekee kuweka uwiano bayana kati ya imani na utamaduni. Kanisa limeendelea
kutumia tamaduni mbali mbali ili kuwatangazia Watu wa Mataifa Habari Njema ya Wokovu,
tangu wakati wa Wagriki.
Kanisa likajifunza Falsafa na mbinu za elimu, lakini
likawa huru kutupilia mbali mambo ambayo yalikuwa yanasigana na imani; na tamaduni
nyingi zikaguswa na kweli za Kiinjili, kwa kuchukua tunu bora na kuacha makapi! Hivi
ndivyo ilivyo pia hata katika matumizi ya mitandao ya kijamii, kuna mambo mazuri yanayopaswa
kuchukuliwa na kuenziwa na Mama Kanisa, lakini pia kuna hatari zinazopaswa kuepukwa.
Kwa kuongozwa na Roho Mtakatifu waamini wanaweza kung'amua fursa zinazopatikana katika
mchakato wa kuutafuta uso angavu wa Kristo.
Baba Mtakatifu anasema, hili ni
jukwaa makini la Uinjilishaji, ingawa haitoshi kuwa na teknolojia tu, bali kujenga
na kudumisha mchakato utakaowawezesha watu kukutana; hawa ni wale ambao wamepoteza
dira na njia; watu ambao wamejeruhiwa; ili waweze kuonjeshwa matumaini mapya.
Utangazaji
wa Injili unahitaji watu kujenga na kudumisha uhusiano wa dhati na Kristo na kwamba,
uwepo wa Kanisa katika mitandao ya kijamii ni muhimu sana. Hapa ni maskani ya maisha
ya vijana, wanaopaswa kusaidiwa ili kuamsha ndani mwao maana ya maisha kwa kuwaonjesha
huruma ya Mungu inayojifunua kwa njia ya Yesu Kristo, Neno wa Mungu aliyefanyika mwili!