2013-12-07 11:35:29

Miaka 80 tangu Mtakatifu Bernadetha Soubirous alipotangazwa kuwa Mtakatifu: Changamoto: maisha ya Sala, Sakramenti na huduma kwa jirani!


Ilikuwa ni tarehe 8 Desemba 1933 wakati Baba Mtakatifu Pio wa kumi na moja alipomtangaza Mwenyeheri Bernadetha Soubirous kuwa Mtakatifu. Ni msichana kutoka Ufaransa aliyebahatika kutokewa na Bikira Maria mara kadhaa kati ya tarehe 11 Februari na tarehe 16 Julai 1858 mjini Lourdes.

Kanisa nchini Ufaransa linaadhimisha Jubilee ya Miaka 80 tangu Bernadetha alipotangazwa kuwa Mtakatifu. Hili ni tukio ambalo linakuwakusanya maelfu ya mahujaji kutoka sehemu mbali mbali za dunia wanaoendelea kumiminika mjini Lourdes, kumwimbia Bikira Maria utenzi wa sifa na shukrani kwa matendo makuu aliyoyafanya miongoni mwa watoto wake hapa duniani.

Maadhimisho haya yameanza tangu Ijumaa kwa Ibada na Tamasha la Muziki; Maandamano ya waamini wakiwa na mianga ya moto, alama za matumaini hadi kwenye Kanisa la Moyo Mtakatifu wa Yesu, mahali ambapo masalia ya Mtakatifu Bernadetha yamehifadhiwa. Kilele cha Maadhimisho haya ni wakati wa Sherehe ya Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili, Jumapili, tarehe 8 Desemba 2013.

Kwa njia ya maombezi ya Mtakatifu Bernadetha, Mama Kanisa anawalika waamini kusonga mbele kwa imani na matumaini, wakidumu katika ukweli na ushuhuda amini katika imani kwa Kristo na Kanisa lake. Wawe ni watu wanaojikita katika maisha ya Sala, Sakramenti za Kanisa na huduma ya upendo kwa jirani.







All the contents on this site are copyrighted ©.