2013-12-06 14:50:07

Wanataalimungu mnapofundisha, msizime moto wa utakatifu wa maisha na ibada!


Baba Mtakatifu Francisko, Ijumaa tarehe 6 Desemba 2013 amekutana na kuzungumza na wajumbe wa Tume ya Kitaalimungu Kimataifa iliyohitimisha mkutano wake wa mwaka hapa mjini Vatican. Baba Mtakatifu amewashukuru wanataalimungu kwa mchango wao mkubwa katika maisha na utume wa Watu wa Mungu. Mkutano huu umeongozwa na kauli mbiu "Taalimungu leo hii, matumaini, kanuni na vigezo".

Taalimungu ni sayansi na hekima inamwezesha mwanadamu kutumia rasilimali mbali mbali kwa ajili ya kutafakari Fumbo la Mungu lililofunuliwa kwa njia ya Yesu Kristo na kwa kujifunza kutoka katika shule ya Bikira Maria aliyehifadhi yote katika sakafu ya moyo wake mtakatifu. Mwanataalimungu ana kazi ya kuunganisha mpango wa Mungu na ukweli wa kiimani. Ni mtu anayetakiwa kusikiliza kwa makini, kufanya mang'amuzi ili hatimaye, aweze kutafasiri mambo yote haya kadiri ya lugha ya watu wa nyakati hzi mintarafu mwanga wa Neno la Mungu.

Wanataalimungu ni waasisi wa majadiliano kati ya Kanisa na tamaduni, ili watu kutoka katika mataifa, lugha, jamaa na lugha, waweze kulipokea Neno la Mungu. Wanataalilimungu hao katika mkutano wao wamejadili kuhusu dini zinazo amini Mungu mmoja pamoja na vurugu za kidini, kwa kutambua kwamba, Imani kwa Mungu mmoja haiwezi kuwa ni chanzo cha vurugu na kinzani za kidini na kijamii, bali iwe ni kikolezo cha upendo na mshikamano kati ya watu, kwani kwa njia mateso, kifo na ufufuko wake, Yesu ameupatanisha ulimwengu wote pamoja na Mwenyezi Mungu.

Baba Mtakatifu anasema, Mafundisho Jamii ya Kanisa yanajikita katika Neno la Mungu, linalopokelewa, linaloadhimishwa na kumwilishwa na Mama Kanisa. Huu ni ujumbe unaopaswa kwanza kabisa kumwilisha ndani ya Kanisa na baadaye, kuwa ni sehemu ya ujumbe wa kijamii kwa ajili ya dunia. Watu wajenge na kudumisha udugu kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii. Uongozi, uthaminiwe na kutambulika kuwa ni huduma na mshikamano na maskini.

Baba Mtakatifu anakumbusha kwamba, Watu wa Mungu wanachangamotishwa kutolea ushuhuda wa kinabii, kwa kukubaliana na kweli za kiimani, daima wakijitahidi kujisikia kuwa ni sehemu ya Kanisa, ili kuendana na kile ambacho kinafundishwa na Imani ya kitume na roho ya Kiinjili. Waamini wanapaswa kuwa na kanuni zinazowasaidia kutambua kweli za kiimani na kwamba, Kanisa halina budi kusikiliza kile ambacho Roho Mtakatifu anataka kutoka kwa Kanisa; jambo muhimu sana kwa wanataalimungu.

Baba Mtakatifu Francisko anawakumbusha wanataalimungu kwamba, kazi yao ni ya maana sana, lakini pia wanakabiliana na hatari kubwa. Tafiti na ufundishaji wa Taalimungu inaweza kuwa ni sehemu ya mchakato wa utakatifu wa maisha, lakini pia inaweza kuwa ni chanzo cha vishawishi: ugumu wa moyo, majivuno na tamaa ya madaraka. Majalimu wa taalimungu wawe makini wanapofundisha ili wasizime moto wa utakatifu wa maisha na ibada.







All the contents on this site are copyrighted ©.