2013-12-06 08:10:15

Tume ya Kipapa kwa ajili ya kulinda na kuwatetea watoto kuanzishwa hivi karibuni!


Baba Mtakatifu Francisko ameamua kuanzisha tume maalum ya kipapa itakayoshughulikia masuala ya kuwalinda watoto dhidi ya nyanyaso za kijinsia na itakuwa na dhamana ya kumshauri mambo muhimu ambayo Kanisa linapaswa kuyatekeleza katika mikakati yake ya kichungaji kwa ajili ya usalama na ustawi wa watoto.

Hayo yamebainishwa na Kardinali Sean Patrick O'Malley, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Boston, Marekani ambaye pia ni mjumbe wa Tume maalum ya Makardinali wanane iliyoundwa na Baba Mtakatifu Francisko ili kumsaidia kupata ushauri wa kufanya mageuzi ndani ya Kanisa. Tume hii imehitimisha kikao chake cha pili, ambacho Baba Mtakatifu Francisko ameshiriki pia. Uamuzi huu ni mwendelezo wa hatua madhubuti zilizokuwa zimeanza kuchukuliwa na Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto wa kumi na sita katika mchakato wa kupambana na nyanyaso za kijinsia zilizokuwa zinafanywa na baadhi ya viongozi wa Kanisa.

Tume itakuwa inamjulisha mara kwa mara Baba Mtakatifu na hatua ambazo Baraza ya Kipapa kwa kushirikiana na Mabaraza ya Maaskofu Katoliki pamoja na Mashirikisho ya Wakuu wa Mashirika ya Kitawa na Kazi za kitume wanayopaswa kuchukua. Tume hii itawashirikisha: Walei, Watawa na Mapadre, watakaokuwa na dhamana ya kulinda na kutetea utu na heshima ya watoto; kujenga uhusiano wa karibu na waathirika pamoja na kuwasaidia kupata tiba muafaka na utekelezaji wa sheria husika. Tume hii itatangazwa na Baba Mtakatifu ikiambatana na Hati maalum ya shughuli za kichungaji.

Kwa upande wake, Padre Federico Lombardi, msemaji mkuu wa Vatican amebainisha kwamba, mkutano wa Tume ya Makardinali awamu ya pili umehitimishwa kwa ushiriki wa Baba Mtakatifu Francisko. Mkutano mwingine wa Makardinali hao wanane utafanyika tena kuanzia tarehe 17 hadi tarehe 19 Februari 2014. Kutafuatia Baraza la Makardinali litakaloanza kikao chake tarehe 20 hadi 21 Februari 2014 na Makardinali wapya watatangazwa hapo tarehe 22 Februari, wakati wa Maadhimisho ya Siku kuu ya Ukulu wa Mtakatifu Petro na Jumapili tarehe 23 Februari 2014, Makardinali wapya wataadhimisha kwa pamoja Fumbo la Ekaristi Takatifu, kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican.

Padre Lombardi anasema, tarehe 24 hadi 25 Februari 2014, Sekretarieti kuu ya Sinodi ya Maaskofu itakuwa na kikao chake hapa mjini Vatican, kama sehemu ya maandalizi ya Maadhimisho ya Sinodi ya Maalum ya Maaskofu kwa ajili ya Familia, itakayofanyika mjini Vatican mwezi Oktoba, 2014.







All the contents on this site are copyrighted ©.