Tata Madiba atakumbukwa kwa kusamehe na kusahau bila kuweka kinyongo moyoni mwake!
Marehemu Nelson Mandela ni kiongozi aliyekuwa na busara na ukomavu, kiongozi ambaye
kwa hakika ni kielelezo cha zawadi ya Mwenyezi Mungu kwa watu wa nyakati hizi. Atakumbukwa
kutokana na jitihada zake za kutaka kuwaunganisha wananchi wa Afrika ya Kusini, waliokuwa
wamegawanyika kutokana na ubaguzi wa rangi; ni kiongozi na mtetezi wa haki msingi
za binadamu, aliyetanguliza utu wa watu kuliko hata masilahi yake binafsi, akawa ni
mfano wa kuigwa dhidi ya ukoloni, ukandamizaji na ubaguzi wa rangi.
Ni sehemu
ya salam za rambi rambi kutoka kwa Dr. Olav Tveit, Katibu mkuu wa Mabaraza ya Makanisa
Ulimwenguni wakati huu dunia inapoomboleza kifo cha Mzee Madiba, kilichotokea Alhamisi,
tarehe 5 Desemba, 2013 mjini Johanesburg, Afrika ya Kusini. Ni kiongozi aliyeonesha
moyo wa shukrani kwa wote waliosaidia kufanikisha mageuzi na uhuru wa kweli nchini
Afrika ya Kusini.
Kanisa lilimsindikiza hata gerezani alipokuwa anatumikia
kifungo cha maisha! Miaka 95 ya Mzee Madiba ni kielelezo cha utu na uhuru wa binadamu
wote, atakumbukwa kwa kusamehe na kusahau bila kuweka kinyongo moyoni, jambo ambalo
si rahisi sana kwa watu wa kizazi hiki wanaotaka kulipiza kisasi. Ni kiongozi na mfano
wa kuigwa katika kusimama kidete kulinda na kutetea misingi ya haki, amani na utu
wa mwanadmu.