Tata Madiba alijisadakisha kwa ajili ya utu na heshima ya binadamu!
Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Bwana Ban Ki-Moon anasema amepokea kwa majonzi makubwa
habari za kifo cha Mzee Madiba, Nelson Mandela, Rais mstaafu wa Afrika ya Kusini,
aliyesimama kidete kutetea haki msingi za binadamu; mfungwa wa dhamiri, ambaye kamwe
hakulalamika hata baada ya kukosewa haki zake msingi; alikuwa ni mtetezi wa haki kimataifa,
Rais wa kwanza mzalendo na mfano wa kuigwa na wengi!
Katibu mkuu wa Umoja wa
Mataifa, kwa niaba ya Umoja wa Mataifa anapenda kutuma salam zake za rambi rambi kwa
wananchi wa Afrika ya Kusini na kwa namna ya pekee kwa familia yake. Watu wengi duniani
waliguswa na kuhamasishwa na sadaka kubwa iliyotolewa na Mzee Madiba katika kulinda
na kutetea: utu, heshima, usawa na uhuru wa kweli. Ni mfano wa pekee katika Jumuiya
ya Kimataifa katika kutetea mafao ya wengi kwa ari na moyo mkuu.
Bwana Ban
Ki-Moon anasema, Mzee Madiba ameonesha kwamba, inawezekana watu kufanya kazi kwa umoja,
upendo na mshikamano wa dhati kwa ajili haki na utu wa mwanadamu. Kanuni maadili ilimsukuma
kupinga vitendo vyote vya ubaguzi wa rangi na baada ya kuporomoka kwa utawala wa ubaguzi
wa rangi, akaanzisha mchakato wa majadiliano, haki na amani; ukweli na uptanisho.
Ni kiongozi aliyejisadaka kwa ajili ya haki msingi za binadamu, mchango ambao
wengi wameshiriki hata bila kujitambua kama alivyosema Tata Madiba alipokutana na
Bwana Ban Ki-Moon siku moja!