Tafakari ya Neno la Mungu, Jumapili ya Pili ya Kipindi cha Majilio
Tunaendelea katika kushirikishana meza ya Neno la Mungu, tayari tukiwa katika Dominika
ya II ya Majilio mwaka A.
Neno la Mungu
ndiyo dira na taa ya maisha yetu. Mwaliko wa Neno la Mungu Dominika iliyopita ulikuwa
ni kukesha na kusali kwa maana hatujui siku wala saa atakayokuja Bwana wetu, na Dominika
hii tunaalikwa KUTAYARISHA NJIA YA BWANA.
Katika mantiki ya kutayarisha njia
ya Bwana yatupasa kufikiri kwa nini tunaalikwa kufanya hivyo? Tunaalikwa kutenda hivyo
kwa sababu Masiha ajaye ni kiongozi na mfalme wa mbingu na dunia, kumbe hatuna budi
kumkaribisha. Huyu kiongozi ajaye, katika somo la I anajulikana kama tawi litakalochipuka
katika shina la Yese. Sifa yake ya pekee, anayo hekima na ufahamu wa pekee kwa ajili
ya kazi yake ya wokovu.
Mpendwa mwana wa Mungu, ujumbe wa kutayarisha njia
ya Bwana, unaletwa kwetu na Nabii Yohane Mbatizaji ambaye anatoa sauti ya kutangaza
akiwa jangwani. Mwaliko wa Yohane Mbatizaji uko katika TOBA kwa ajili ya kutayarisha
mioyo yetu ili kumpokea Mungu. Yohane Mbatizaji anapotangaza ujumbe huu anaturudisha
nyuma kidogo katika maneno ya Nabii Isaya anayeishi katika karne ya 8 hivi kabla ya
Kristu asemaye: sauti ya mtu aliaye nyikani, itengenezeni njia ya Bwana, yanyosheni
mapito yake.
Ndiyo kusema Yohane Mbatizaji anakazia na kuyaweka katika matendo
mausia ya Mungu kwa njia ya Nabii Isaya. Yohane anataka watu wafunge na kwa njia hiyo
wafungue mioyo yao tayari kwa wokovu. Anakazia kuwa wokovu hauji kwa njia ya miujiza
bali lazima mmoja aongoke na kuifuata njia ya Bwana. Anataka watu waungame dhambi
zao, kama ambavyo twafahamu jinsi walivyomwendea watu wa zama hizo pale katika mto
Yordani.
Mpendwa msikilizaji, mwaliko wa Yohane Mbatizaji katika majilio haya
ni toba inayogeuza maisha yetu kwa dhati kabisa bila kurudi nyuma. Toba anayoidai
Yohane ni ile inayokuza jina la Bwana kwa njia ya unyenyekevu, kama yeye alivyotangaza
wazi kuwa yeye hasitahili kugusa hata kamba za viatu vya Bwana ajaye yaani Masiha.
Katika somo la pili Mtume Paulo anaweka sala kwa ajili yetu akisema “Mungu
awajalieni kuwa na msimamo mmoja kufuatana na mfano wake Kristu Yesu. Msimamo wake
Yesu uwe msimamo wetu na zaidi ya yote fadhila ya upendo kwa watu ikomae. Kumbe kutayarisha
njia ya Bwana ni katika kueneza upendo kwa watu wa Mungu. Kila mmoja anayejaribu kuweka
maisha yake kwa ajili ya wengine anakuwa Kristu mwingine aliyejitoa maisha yake kwa
ajili ya ulimwengu.
Basi mpendwa msikilizaji, jiwekeni daima katika usikivu
ili maneno ya Yohane Mbatizaji na Mt. Paulo yawe chakula chako cha kila siku na hiyo
ndiyo namna ya kuishi majilio ukitayarisha njia ya Bwana.
Nikutakie Dominika
njema na majilio njema katika kujiweka tayari kwa kuzaliwa Mtoto Emanueli. Tumsifu
Yesu Kristo na Bikira Maria.
Tafakari hii imeletwa kwako na Pd Richard Tiganya,
C.PP.S.