Baba Mtakatifu Francisko, Ijumaa, tarehe 6 Desemba 2013 amekutana na kufanya mazungumzo
ya faragha na Bwana Antonio Guterres, Kaminishina wa Shirika la Umoja wa Mataifa
kwa ajili ya Wakimbizi. Hadi sasa kuna jumla ya wakimbizi millioni 45 wanaolazimika
kuzikimbia nchi zao kutokana na sababu mbali mbali.
Bwana Guterres ametumia
fursa hii kumshukuru Baba Mtakatifu Francisko kwa kuguswa sana na mahangaiko pamoja
na mateso ya wakimbizi wanaotafuta nafuu na ubora wa maisha, lakini kwa bahati mbaya
wanakumbana na kifo hata kabla ya kufika kwenye nchi ambazo wanadhani kuna matumaini
ya maisha bora zaidi! Wakimbizi kwa sasa wanakabiliana na vikwazo vingi kutokana na
sababu kwamba nchi nyingi zimeweka sheria ngumu kama njia ya kudhibiti wakimbizi na
wahamiaji kupata hifadhi.
Takwimu zinaonesha kwamba, idadi kubwa ya wakimbizi
ni wale wanaotoka Syria, Eritrea na Somalia, ambao wengi wao wanapoteza maisha kwa
kufa maji baharini. Bwana Gutteres anasema, kuna haja kwa nchi za Ulaya kujenga mazingira
ambayo yatawezesha wakimbizi kupokelewa na kupata hifadhi, kwa kuzingatia sheriam,
kanuni na misingi ya Jumuiya ya Kimataifa.
Shirika la Wakimbizi la Umoja wa
Mataifa kwa sasa linaendelea kuimarisha kikosi cha uokoaji sanjari na kudhibiti biashara
haramu ya binadamu inayofanywa na baadhi ya watu wenye uchu wa mali na utajiri wa
haraka haraka, kiasi hata cha kubeza utu na heshima ya binadamu wenzao. Shirika hili
pamoja na mambo mengine limeanza kutekeleza mikakati ya kuwalinda wakimbizi mara wanapowasili
katika nchi kavu!
Baba Mtakatifu pamoja na mgeni wake, wameguswa kwa namna
ya pekee na hali ngumu ya wakimbizi kutoka Syria pamoja na kuibua mbinu mkakati wa
kusaidia nchi jirani zinazopokea wakimbizi kutoka Syria, ambao kwa sasa idadi yao
imefikia kiasi cha wakimbizi millioni mbili. Inasikitisha kusikia kwamba, kuna baadhi
ya nchi zinaanza kujiwekea mikakati ya kutokubali tena kupokea na kutoa hifadhi kwa
wakimbizi na wahamiaji wanaotaka kuokoa maisha yao.
Bwana Guterres anasema,
viongozi wa Kidini wanao mchango mkubwa katika mchakato wa kuwasaidia wakimbizi na
wahamiaji wanaotafuta nafuu ya maisha ugenini. Viongozi wa kidini wamekuwa mstari
wa mbele kuhimiza Serikali zao kutoa hifadhi kwa wakimbizi sanjari na kutokomeza hali
ya kutovumiliana na nyanyaso za kibaguzi ambazo hazina tena tija wala mashiko kwa
Jumuiya ya binadamu ambayo kwa sasa inaishi kama Kijiji.