2013-12-06 10:24:08

Endeleeni kumuenzi Tata Madiba kwa kusimama kidete kutetea haki, uhuru, usawa, demokrasia kwa kupinga rushwa na ufisadi!


"Haya na tuwasifu watu wa utauwa, na baba zetu katika vizazi vyao. Bwana aliwafanyizia utukufu mwingi, waliomashuhuri tangu siku za kale. Wale waliotawala katika milki zao, maarufu kwa kuwa walikuwa hodari kwa ushauri, mafundisho na akili zao na kuhubiri mambo kwa unabii wao!

Kwa maneno haya kutoka katika Kitabu cha Hekima ya Yoshua Bin Sira, Shirikisho la Mabaraza la Maaskofu Katoliki Kusini mwa Afrika linapenda kutoa salam zake za rambi rambi kutokana na kifo cha Tata Nelson Mandela kilichotokea siku ya Alhamisi, tarehe 5 Desemba 2013. Wananchi wa Afrika ya Kusini wanamkumbuka Mzee Madiba aliyejisadakisha kwa ajili ya mafao ya wananchi wa Afrika ya Kusini; akawaongoza katika mchakato wa haki, amani na upatanisho wa kitaifa.

Ni kiongozi aliyesimama kidete kupinga ubaguzi wa rangi Afrika ya kusini, akawa Rais wa kwanza Mzalendo kuanzisha mchakato wa demokrasia ya kweli, inayojikita katika: haki, uhuru na usawa. Tata Madiba amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 95.

Askofu mkuu Stephen Brislin, Rais wa Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Kusini mwa Afrika anasema, Tata Madiba alipoachiliwa huru tarehe 11 Februari 1990, nchi ikaanza kupata mwelekeo mpya, mauaji ya watu wasiokuwa na hatia yakaanza kusitishwa. Kunako Mwaka 1994 alipochaguliwa kuwa ni Rais wa Afrika ya Kusini, akaanzisha mchakato wa upatanisho, haki na amani, akawataka wananchi wa Afrika ya Kusini kuachana na mauaji ya watu wasiokua na hatia! Huu ndio ujumbe endelevu hata wakati huu.

Wananchi wa Afrika ya Kusini wanaweza kumuenzi Tata Madiba kwa kusimama kidete kulinda na kutetea haki msingi za binadamu, uhuru, usawa, demokrasia pamoja na kupinga rushwa na ufisadi.







All the contents on this site are copyrighted ©.