2013-12-06 14:53:31

Cheche za mageuzi ya utakatifu ndani ya Kanisa zinafumbata: toba na wongofu wa ndani; Neno la Mungu na matendo ya huruma!


Baba Mtakatifu Francisko, Makardinali, Maaskofu na Wakuu wa Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kitume, Ijumaa tarehe 6 Desemba 2013 wameshiriki katika mahubiri ya Kipindi cha Majilio, yaliyotolewa na Padre Raniero Cantalamessa, mhubiri mkuu wa Nyumba ya Kipapa, kwa kuongozwa na kauli mbiu: Mtakatifu Francisko wa Assisi na Mageuzi ndani ya Kanisa kwa njia ya Utakatifu wa Maisha. Mtakatifu Francisko kwa njia ya ushuhuda wa utakatifu wa maisha, aliweza kuchangia kuleta mageuzi makubwa katika maisha na utume wa Kanisa.

Padre Cantalamessa katika tafakari yake amegusia mambo makuuu matatu: kwanza ni toba na wongofu wa ndani uliofanywa na Mtakatifu Francisko; Pili mchango wa Mtakatifu Francisko wa Assisi katika kuleta mageuzi ndani ya Kanisa; tatu Mtakatifu Francisko na umuhimu wa Injili kama chachu ya mageuzi ndani ya Kanisa na mwishoni, ameonesha baadhi ya mambo ambayo Kanisa katika ulimwengu wa utandawazi linaweza kufuata ili kuharakisha mageuzi ya maisha na utume wa Kanisa yaliyoanzishwa na Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican.

Toba na wongofu wa ndani ni mambo yaliyomwezesha Mtakatifu Francisko kushikamana na wagonjwa pamoja na maskini, ili kuwaonjesha huruma na upendo wa Mungu! Hakuchagua umaskini, bali maskini, ili kutekeleza amri ya upendo kwa Mungu na jirani, kwa njia hii akawaonjesha upendo wa Kristo hata katika umaskini wao, akamua kuubeba Msalaba wake, ili kumfuasa Kristo kwa ukaribu zaidi, ili hatimaye, huruma ya Mungu iweze kupata ushindi mkamilifu.

Hivi ndivyo walivyofanya hata akina Mtume Paulo, mwalimu wa mataifa, akaamua kumpatia Kristo kipaumbele cha kwanza katika maisha na utume wake, akawa kweli ni cheche ya toba na wongofu wa ndani kwa Kanisa.

Padre Cantalamessa anasema kwamba, Mtakatifu Francisko aliishi katika nyakati ambamo kulikuwa na kinzani kubwa kati ya Kanisa na Viongozi wa Serikali; Kanisa likawa linajitafuta kwa ajili ya masilahi yake binafsi na kusahau dhamana ya kuokoa roho za watu. Huu ukawa ni mwanzo wa kuibuka kwa Mashirika ya Kitawa. Lakini watu wengi walianza kuhamia mijini wakitafuta uhuru zaidi. Kanisa kwa wakati huo lilikuwa limekumbatia utajiri mkubwa ambao ulikuwa pia ni sababu ya kinzani na chokochoko za kijamii.

Mtakatifu Francisko akaibuka kama cheche ya mageuzi ndani ya Kanisa kwa kuchagua Nadhiri ya Ufukara, kama kielelezo makini cha kumfuasa Yesu, kama lilivyokuwa Kanisa la Mwanzo, lililoshikamana kwa dhati kwa njia ya tafakari ya Neno la Mungu na matendo ya huruma. Mtakatifu Francisko akafanya mageuzi ndani ya Kanisa kwa njia ya Utakatifu wa maisha, tofauti na Luteri aliyejitoa na kuanzisha Kanisa lake.

Huu ukawa ni mwanzo mwingine wa kuibuka kwa Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kitume kwa ajili ya kukoleza Utakatifu wa maisha na hivyo kuleta mageuzi ya kweli katika maisha na utume wa Kanisa. Mtakatifu Francisko akashiriki kikamilifu katika ujenzi wa Kanisa la Kristo lililokua limechakaa kutokana na mapungufu ya kibinadamu!

Padre Cantalamessa anasema kwamba, Injili ilikuwa ndiyo chachu ya mabadiliko makubwa katika maisha yake, akawachangamotisha wengine kusoma, kutafakari na kumwilisha Neno la Mungu katika maisha yao, kama kielelezo cha ushuhuda amini. Akahubiri umuhimu wa kufanya toba na wongofu wa ndani, kama njia ya kuiamini Injili ya Kristo.

Huu ndio mwaliko ulioletwa tena na Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican, kwa kulitaka Kanisa kuwa ni mhudumu na sauti ya wanyonge na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii. Kanisa likawa mstari wa mbele kukumbatia umuhimu wa majiundo ya mtu mzima: kiroho na kimwili. Sala za Kanisa zikapewa msukumo wa pekee kwa watu wa Mungu. Mtakatifu Francisko hakuona sayansi kuwa ni kikwazo kwa Sala na tafakari ya Neno la Mungu. Mageuzi ya kweli yanafanywa kwa njia ya mshikamano wa dhati kama anavyosema Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka wake wa Kitume, Injili ya Furaha.

Padre Cantalamessa anasema, utakatifu wa maisha ni njia msingi katika kuendeleza mchakato wa mageuzi ndani ya Kanisa. Waamini wakubali kuufia ulimwengu na kamwe wasimezwe na malimwengu. Utakatifu uanze katika maisha ya binafsi kwa kubeba Msalaba na kuanza kumfuasa Kristo Mkombozi wa dunia. Kristo na Kanisa lake, wapewe kipaumbele cha kwanza, kuliko kutafuta utukufu na masilahi ya binafsi.

Kwa njia ya upendo wa dhati, kila mwamini anaalikwa kuchangia katika ujenzi wa Ufalme wa Mungu. Waamini wawe na ujasiri wa kuvua utu wa kale na kuanza kujivika utu mpya, huku wakitembea katika mwanga wa Kristo, wakijikita katika majadiliano ya kweli kwa kuendelea kutangaza Injili ya Furaha kwa njia ya upendo mkamilifu na huo utakuwa ni mwanzo wa amani ya kweli katika sura ya nchi.







All the contents on this site are copyrighted ©.