2013-12-06 08:59:46

Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili


Mama Kanisa hapo tarehe 8 Desemba 2013 ataadhimisha Sherehe ya Bikira Maria kukingiwa Dhambi ya Asili. Baba Mtakatifu Francisko anatarajiwa kama yalivyo mapokeo, kwenda kwenye Uwanja wa Spagna, ulioko mjini Roma ili kuweka shada la maua kwenye Sanamu ya Bikira Maria iliyowekwa uwanjani hapo. RealAudioMP3

Mafundisho haya tanzu ya Kanisa yalitangazwa na Baba Mtakatifu Pio wa tisa kunako Mwaka 1854, akionesha kwamba, Bikira Maria kukingiwa dhambi ya asili ni upendeleo wa pekee kutoka kwa Mwenyezi Mungu, kwa kutazamia masthahili ya Yesu Kristo, mkombozi wa dunia, alikingiwa kila doa la dhambi ya asili.Ni Mama wa Mungu na wa Kanisa.

Sr. Maximillian Immaculata wa Shirika la Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili kutoka Tanzania anasema, kwa watawa, hii ni sherehe ya pekee kwani Bikira Maria ni Mama, kiongozi, msimamizi na mwombezi wa watawa wote, bila kuisahau Familia yote ya Mungu. Bikira Maria ni mfano bora wa kuigwa na watawa wote kwani alijiachilia mikononi mwa Mwenyezi Mungu, akisema, "mimi ni mtumishi wa Bwana, na iwe kwangu kama ulivyo nena".

Kwa utayari huu, Bikira Maria amekuwa ni Mama wa Yesu na Kanisa, Mama wa Watawa wote wanaomfusa Kristo kwa njia ya Mashauri ya Kiinjili, kwa ajili ya Mungu na Jirani zao. Bikira Maria alikumbatia ndani mwake mapenzi ya Mungu, changamoto kwa watawa kutafuta na kuyatenda mapenzi ya Mungu katika maisha na utume wao, tayari kujitosa kimasomaso kushiriki kikamilifu katika kazi ya Ukombozi na ujenzi wa Ufalme wa Mungu hapa duniani.







All the contents on this site are copyrighted ©.