2013-12-05 13:51:21

Zitto amrushia "dongo" Waziri Mkuu Pinda


Waziri Mkuu wa Tanzania Mizengo Pinda amesema yeye ni kinara wa kukopa na kamwe hapokei mshahara mkubwa kama inavyodaiwa na baadhi ya watu akiwemo mbunge wa Kigoma Zitto Kabwe. Pinda alisema mshahara wake kwa mwezi ni sh. Milioni sita na si milioni 30 kama alivyodai mbunge Zitto.

‘’Mimi napokea shilingi milioni sita kama mshahara wangu na posho ya mke wangu, sasa ninaposikia napokea milioni 30 nilishangaa kweli nikaona mtu huyu alisema hivyo nikamshangaa’’ alisema Pinda.

Pinda alisema pamoja na yeye kupokea kiasi hicho bado viongozi wa juu yake nao hawapokei kiasi kikubwa kama inavyofikiriwa na wengi. Alisema tofauti ya mshahara wake na Makamu wa Rais haitofautiani sana kwa kuwa tofauti yake ni katika ya sh. Milioni moja.

Pinda alisema yeye binafsi ni kinara wa kukopa kwa ajili ya matumizi yake mbalimbali kwani ameshakopa katika Benki za NMB na CRDB. “ Na hata hapa karibuni mlipotoa ruhusa ya kukopa kiinua mgongo mimi nimekopa asilimia 50 ya kiinua mgongo changu, sasa kama ningekuwa na mashahara mkubwa kiasi hicho cha milioni 30 nisingelazimika kufanya hivyo’’ alisema Pinda.

Alisema fedha zingine anazopata ni pamoja na posho za ubunge kama wanazopata wabunge wengine ambazo ni kati ya sh. 500,000 na 600,000. Waziri Pinda alisema wanashukuru uongozi uliopita wa nchi kuweka utaratibu wa kuwahudumia viongozi wake kwa kuwapa nyumba za kuishi bure na kupata chakula bure. “ Kama kuna nchi imeweka utaratibu mzuri katika kuwahudumia viongozi wake basi Tanzania ni moja wapo lazima tuwashukuru Watanzania katika kufikiria hilo’’ alisema Pinda.

Pinda alikuwa akijibu swali la mbunge wa Mkanyageni Mohamed Habib Mnyaa (CUF) aliyetaka kujua Waziri Mkuu anapokea mshahara kiasi gani na pia kama mshahara huo umepitishwa na Bunge. Aidha Waziri Mkuu amesema serikali ina imani kuwa utaratibu wa kutumika kwa vitambulisho vya utaifa katika uchaguzi mkuu hujao unawezekana.

Pinda alisema kwa sasa zoezi hilo linaendelea vyema kwani lilikuwa likisusua kufuatia mchakato wa Sheria ya manunuzi, lakini kwa sasa utaratibu wa utoaji wa vitambulisho hivyo unaendelea vizuri na wanatarajia vitambulisho hivyo kutumika kama ilivyotakiwa. Pinda alikuwa akijibu swali la Rajab Mbarouk Mohamed (Ole) aliyetaka kujua kama serikali itaweza kukamilisha taratibu za utoaji wa vitambulisho hivyo katika kipindi kilichobaki cha kufikia uchaguzi mkuu ujao.








All the contents on this site are copyrighted ©.