Yesu ni mwamba thabiti, dira na nguzo ya maisha ya waamini inayopaswa kushuhudiwa
kwa matendo zaidi!
Waamini wanatakiwa kusikiliza kwa makini, kulitafakari Neno la Mungu na hatimaye,
kulimwilisha katika maisha na vipaumbele vyao, kwa kutambua kwamba Yesu Kristo ni
mwamba imara wa maisha, kiini na chemchemi ya umoja, upendo na mshikamano wa dhati.
Haitoshi kuzifahamu Amri za Mungu, bali kuzitekeleza na kuzimwilisha katika
uhalisia wa maisha ya kila siku. Neno la Mungu ni msingi thabiti ambao waamini wanaweza
kujenga maisha yao juu yake, bila wasi wasi wowote!
Ni sehemu ya mahubiri yaliyotolewa
na Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Ibada ya Misa Takatifu, Alhamisi, tarehe 5 Desemba,
2013 kwenye Kikanisa cha Mtakatifu Martha kilichoko mjini Vatican. Anasema, Yesu ni
mwamba thabiti na chemchemi ya maisha ya waamini, kiasi kwamba, wanaweza kusonga mbele
pasi na mashaka. Neno la Kristo halina budi kumkumbatia Yesu Kristo mwenyewe, vinginevyo
kuna hatari kubwa. Waamini hawana budu kuhakikisha kwamba, maneno na matendo yao yanaonesha
ile imani yao kwa Kristo na Kanisa lake, katika unyenyekevu kama alivyofanya Bikira
Maria.
Yesu awe ni mwamba, dira na nguzo ya maisha ya waamini si tu kwa maneno
bali kwa njia ya ushuhuda wa imani tendaji. Waamini wajenge uhusiano wa karibu zaidi
na Kristo kwa njia ya Neno, Sakramenti na Matendo ya huruma, kama kielelezo cha kuwashirikisha
wengine upendo unaobubujika kutoka kwa Kristo na Kanisa lake. Waamini wajenge maisha
na familia zao katika Mwamba thabiti ambao ni Yesu Kristo Mkombozi wa dunia. Ni changamoto
kwa waamini kuchunguza dhamiri zao na kuona ikiwa kama maneno wanayokiri kwa vinywa
vyao yanakwenda sanjari na matendo yao ya Kikristo.
Unyenyekevu uwawezeshe
waamini kusonga mbele ili kutangaza matendo makuu ya Mungu, vinginevyo, kiburi na
majivuno yanaweza kuwasababishia majanga ya kiimani!