2013-12-05 11:25:54

Watu wanamiminika mjini Vatican ili: kumwona, kumsikiliza na kumwombea Papa Francisko mtu wa watu!


Sr. Maximilliana Immaculata wa Shirika la Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili kutoka Tanzania anasema kwamba, amefurahi kushiriki katika Katekesi ya Baba Mtakatifu Francisko, Jumatano tarehe 4 Desemba 2013 na hivyo kuungana na maelfu ya watu wanaomiminika kila siku mjini Vatican ili kumwona, kumsikiliza na kumwombea katika maisha na utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro, wakati huu Kanisa linapoendelea kukabiliana na changamoto mbali mbali kutoka katika ulimwengu wa utandawazi. RealAudioMP3

Anasema, alipokuwa kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican amejisikia kuwa na amani ya ndani, faraja, imani na nguvu ya kusonga mbele katika maisha na utume wake kama Mtawa. Mwaka wa Imani uliohitimishwa na Mama Kanisa kwa Sherehe za Kristo Mfalme ni mwaliko kwa waamini kumtambua Yesu Kristo kuwa ni Mfalme wao wa maisha, Kiongozi wao mkuu na Mchungaji mwema aliyethubutu kuyamimina maisha yake ili kumkomboa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti.

Mwaka wa Imani imekuwa ni fursa kubwa kwa waamini kuweza kufanya tafakari ya kina kuhusu: Imani wanayoungama na kuikiri kwa vinywa vyao; Imani wanayoadhimisha katika Liturujia na Sakramenti za Kanisa; Imani wanaoishi kadiri ya Amri za Mungu, sheria na kanuni maadili; Imani wanayosali katika Zaburi, lakini zaidi katika Sala mbali mbali za Kanisa na binafsi. Ni mwaliko kwa waamini kuhifadhi utajiri huu ili kuutolea ushuhuda wa kweli!







All the contents on this site are copyrighted ©.