Makardinali walioteuliwa na Baba Mtakatifu Francisko kumsaidia kuchangia mawazo ili
kufanya mageuzi ndani ya Kanisa wanaendelea na mkutano wao mjini Vatican. Makardinali
wameendelea kushirikishana mang'amuzi na mawazo yao katika hali ya utulivu, ukweli
na uwazi kwa ajili ya mafao na maendeleo ya Kanisa.
Kikao cha Jumatano asubuhi,
Baba Mtakatifu Francisko hakuweza kuhudhuria kutokana na sababu kwamba, alikuwa anaendesha
Katekesi kwa mahujaji na wageni waliokuwa wamefurika kwa wingi mjini Vatican. Jumanne
jioni, Askofu mkuu Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican, alialikwa kuonana na kusalimiana
na Makardinali hawa, kwani Askofu mkuu Parolin ni kati ya wasaidizi wakaribu sana
wa Baba Mtakatifu.
Padre Federico Lombardi, SJ, msemaji mkuu wa Vatican anabainisha
kwamba, Makardinali katika mkutano wao, wanaendelea kupembua kwa kina na mapana kuhusu
Mabaraza mbali mbali ya Kipapa na baadaye yatafuata mabaraza ya ushauri na hatimaye,
taasisi za kipapa. Mzunguko huu wa kwanza unachambua mambo muhimu ambayo baadaye yatafanyiwa
kazi kwa utekelezaji zaidi.