Kanisa halina sababu ya kuogopa maendeleo ya sayansi na teknolojia ya mawasiliano!
Baraza la Kipapa kwa ajili ya walei limeanza mkutano wake wa ishirini na sita kwa
Ibada ya Misa Takatifu iliyoongozwa na Kardinali Stanislaw Rylko, Rais wa Baraza la
Kipapa kwa ajili ya walei, unaoongozwa na kauli mbiu "Kumtangaza Kristo katika kipindi
cha digitali". Katika mahubiri yake amewataka wajumbe hawa kuhakikisha kwamba, wanajenga
maisha yao ya Kikristo katika mwamba thabiti ambaye ni Yesu Kristo, kwa kufuata maamuzi
thabiti ya maisha pamoja na kutekeleza mapenzi ya Mungu.
Kardinali Rylko anasema
kwamba, katika ulimwengu wa utandawazi watu wengi wanapenda maisha ya mkato ambao
hayajengwi katika msingi thabiti, lakini waamini wanaalikwa kujenga matumaini yao
kwa Mwenyezi Mungu, chemchemi ya amani na furaha ya kweli. Huu ni mwaliko wa kupokea,
kulitafakari na kulimwilisha Neno la Mungu katika vipaumbele vya maisha, ili liwe
ni dira na mwongozo wa maisha.
Mama Kanisa anatumwa kuwatangazia watu wa kizazi
cha dijitali ujumbe wa amani na matumaini kwa kutumia njia mbali mbali za mawasiliano
ya jamii, sanjari na kutambua kwamba, njia hizi zina mafao yake makubwa, lakini wakati
mwingine zina vivuli na giza linaloweza kuwapoteza watu. Wakristo wawe makini katika
matumizi ya njia za mawasiliano ya kijamii kwa kuonesha utambulisho wao unaojikita
kwa njia ya majadiliano ya kina; kwa kuhamasisha na kutia moyo pasi na kukata tamaa.
Ulimwengu
wa dijitali anasema Baba Mtakatifu Francisko ni changamoto ya kimissionari kwa Wakristo
katika ulimwengu wa utandawazi na maendeleo ya sayansi na teknolojia, ili kuwasaidia
watu waweze kukutana na Yesu anayezima kiu ya undani wa maisha yao. Ili kukabiliana
na changamoto hii, kuna haja ya kuwa na majiundo makini kwa waamini walei ambao ni
wadau wakuu na watumiaji wa mitandao ya kijamii katika maisha yao ya kila siku.
Ikumbukwe
kwamba, ulimwengu wa dijitali unaundwa na wanawake na wanaume, wanaobeba ndani mwao:
matumaini, mahangaiko na wasi wasi wa maisha. Ni watu wanaotafuta kilicho cha kweli,
kizuri na chema. Lakini ikumbukwe kwamba, kila mtu binafsi anaalikwa kukutana na hatimaye,
kuambatana na Yesu katika hija ya maisha yake. Kutokana na ukweli huu, njia za mawasiliano
ya kijamii hazitoshi kufikisha ujumbe wa Injili katika mchakato wa Uinjilishaji mpya;
mtu anapaswa kupewa kipaumbele cha kwanza. Kila Mkristo anapaswa kuhamasika kuwa ni
mtangazaji wa kweli za Kiinjili.
Katika hotuba yake ya ufunguzi, Kardinali
Rylko amempongeza Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto wa kumi na sita kwa utume na maisha
yake, lakini kwa maamuzi machungu aliyoyachukua kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya
Kanisa la Kristo. Ni kiongozi aliyewahamasisha waamini walei kutekeleza wajibu na
dhamana yao katika maisha na utume wa Kanisa, wakitambua kwamba, wanatumwa kuyatakatifuza
malimwengu kwa njia ya ushuhuda wa imani tendaji!
Wanamshukuru Baba Mtakatifu
Francisko kwa kuridhia tena Baraza la Kipapa kwa ajili ya waamini walei kuendelea
na utume wake. Amegusia kuhusu Kongamano la Waamini walei lililofanyika Younde, nchini
Cameroon, Septemba 2012, kama sehemu ya mchakato wa majiundo ya waamini walei ili
waweze kuyafahamu vyema Mafundisho ya Kanisa, tayari kuyatolea ushuhuda, wakitambua
kwamba, wao wanapaswa kuwa ni chumvi na mwanga wa mataifa.
Awamu ya Pili ya
Sinodi ya Afrika na Sinodi ya Uinjilishaji Mpya sanjari na Mwaka wa Imani ni matukio
ambayo yamekuwa na utajiri mkubwa katika maisha na utume wa Kanisa. Siku ya Vijana
Duniania kwa Mwaka 2013 imekuwa na mafanikio makubwa inayowataka vijana kuendelea
kuwa ni watangazaji wa Habari Njema ya Wokovu hadi miisho ya dunia. Maadhimisho haya
ni sehemu ya mchakato wa majiundo makini kwa vijana, yaliyoanzishwa kunako mwaka 1985
na Mwenyeheri Yohane Paulo II. Mwaka 2016, Vijana watakusanyika Jimbo kuuu la Cracovia,
Poland.
Kardinali Rylko anasema, wanawake kwa njia ya semina mbali mbali wameendelea
kujengewa uwezo ili kutambua dhamana na mchango wao wa kimama katika maisha na utume
wa Kanisa. Baba Mtakatifu Francisko katika Maadhimisho ya Mwaka wa Imani amekutana
na vyama mbali mbali vya kitume, akivitaka kushiriki kikamilifu katika mchakato wa
Uinjilishaji mpya kwa kusoma alama za nyakati; kwa kuwa na ari pamoja na mbinu mpya
kwa ajili ya watu wa kizazi hiki. Huu ni wajibu unaofumbatwa kutoka katika Sakramenti
ya Ubatizo.
Njia mpya za mawasiliano ni nyenzo muhimu sana kwa Kanisa katika
kuwafikia watu wengi zaidi, lakini kwa namna ya pekee vijana ambao wanatumia muda
wao mwingi katika mitandao ya kijamii. Vijana hawa watangaziwe Kweli za Kiinjili;
wajengewe jukwaa la majadiliano ili kuondoa wasi wasi na hatimaye, kuimarisha matumaini
yao kwa Kristo na Kanisa lake. Waamini wanahamasishwa kujenga utamaduni wa kusikiliza,
kujadili na kuimarishana ili kutafuta mambo msingi katika maisha.
Tafiti za
kitaalam zinaonesha kwamba, kuna matumizi makubwa ya mitandao ya kijamii yanayofanywa
na vijana kwa ajili ya: masomo, mawasiliano, michezo na kwamba, kuna baadhi ya vijana
wamejikuta wakitumbukia katika hatari za kumezwa na malimwengu yanayosambazwa kwenye
mitandao ya kijamii. Kanisa linapaswa kuonesha uwepo wake wa kinabii kama sehemu ya
mchakato wa Uinjilishaji. Hakuna sababu ya kuogopa maendeleo ya sayansi na teknolojia
ya mawasiliano, kwani kati ya zawadi kubwa ambazo Mwenyezi Mungu amewakirimia watu
wa nyakati hizi ni njia mpya za mawasiliano ya kijamii.
Yesu anapaswa kupewa
kipaumbele cha kwanza katika mchakato mzima wa Uinjilishaji kama njia ya kuwashirikisha
wengine ujumbe wa matumaini, neema na upendo wa Kristo.