Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu, Jakaya Mrisho Kikwete
amewapandisha vyeo Maafisa Wakuu wanne wa Jeshi la Polisi Tanzania. Aidha, Rais Kikwete
amefanya uteuzi wa nafasi za madaraka katika Jeshi hilo kufuatia mabadiliko ya muundo
wa Jeshi la Polisi Tanzania.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa Ikulu, Dar Es
Salaam, Jumanne, Desemba 3, 2013 na Kaimu Katibu Mkuu Kiongozi, Dr. Florens Turuka
waliopandishwa vyeo kuwa Kamishna wa Polisi (CP) na ambao wote walikuwa ni Naibu Kamishna
wa Polisi ni DCP Ernest Mangu, DCP Thobias Andengenye, DCP Abdulrahaman Kaniki na
DCP Hamdan Omari Makame.
Rais pia amempandisha cheo SACP Athuman Diwani kuwa
Naibu Kamishna wa Polisi. Walioteuliwa katika nafasi za madaraka katika Jeshi la Polisi
ni CP Clodwing Mtweve ambaye anakuwa Kamishna wa Fedha na Utaratibu wa Ugavi na Usafirishaji
wa Watu na Vitu (Logistics), CP Paul Chagonja ambaye anakuwa Kamishna wa Operesheni
na Mafunzo, CP Isaya Mungulu ambaye anakuwa Mkurugenzi wa Uchunguzi wa Makosa ya jinai
(DCI), CP Mussa Ali Mussa ambaye ameteuliwa kuwa Kamishna wa Polisi Jamii.
Wengine
ni CP Hamdan Omari Makame ambaye anakuwa Kamishana wa Polisi, Zanzibar; CP Ernest
Mangu ambaye anakuwa Mkurugenzi wa Usalama wa Jinai, CP Thobias Andengenye ambaye
anakuwa Kamishna wa Utawala na Utumishi, CP Abdulrahman Kaniki ambaye anakuwa Kamishna
wa Uchunguzi wa Ushahidi wa Jinai na CP Abdulrahman Diwani ambaye anakuwa Naibu Mkurugenzi
wa DCI.