Tuzo ya heshima kwa Papa mstaafu Benedikto XVI kwa kusimama kidete kulinda na kutetea
maadili na utu wema katika mambo ya fedha na uchumi!
Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto XVI ametunukiwa tuzo ya heshima kwa kusimama kidete
katika kukazia misingi ya maadili na utu wema katika masuala ya fedha na uchumi kwa
ajili ya mafao na ustawi wa binadamu na Baraza la Kipapa la haki na amani. Kanuni
maadili, utu na heshima ya binadamu ni mambo yanayowaunganisha wasomi, wafanyabiashara
na watu wanaojitolea.
Tuzo hii imetolewa wakati wa semina ya kimataifa iliyokuwa
imeandaliwa na Baraza la Kipapa la haki na amani, tangu tarehe 2 Desemba hadi tarehe
4 Desemba, 2013. Siku ya Jumatano, tarehe 4 Desemba 2013, wajumbe wamehudhuria Katekesi
ya Baba Mtakatifu Francisko kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican.
Tukio hili limehudhuriwa na viongozi waandamizi kutoka Vatican.
Baba Mtakatifu
mstaafu Benedikto wa kumi na sita anastahili tuzo hii ya heshima kwa bidii na juhudi
alizozionesha wakati Jumuiya ya Kimataifa ilipojikuta imetumbukia kwenye athari za
myumbo wa uchumi kimataifa; fursa za ajira zikatoweka, Mabenki yakafilisika na viwanda
vikafungwa kutokana na ukata uliosababishwa na ukosefu wa kanuni maadili, utu na heshima
ya binadamu; watu wengi katika masuala ya fedha na uchumi walielemewa na uchu wa kutaka
kupata faida kubwa, hapa ukawa ni mwanzo wa majanga kwa binadamu!