Mshikamano wa kimataifa unahitajika ili kupambana na baa la njaa na umaskini wa hali
na kipato!
Mabadiliko ya tabia nchi ni jambo linalogusa kwa namna ya pekee haki na usawa katika
Jumuiya ya Kimataifa. Athari za mabadiliko ya tabianchi zinaonesha kwamba, kuna umuhimu
kwa Jumuiya ya Kimataifa kushirikiana na kushikamana katika kuibua mbinu muafaka utakaodhibiti
athari za mabadiliko ya tabianchi. Kwanza watu hawana
budi kurekebisha mitindo ya maisha ambayo inachangia kwa kiasi kikubwa kuchafuzi wa
mazingira, lakini zaidi katika harakati za Jumuiya ya Kimataifa kukabiliana na baa
la njaa pamoja na umaskini wa hali na kipato unaoendelea kunyanyasa maisha ya mamillioni
ya watu duniani. Ni mchango wa Askofu mkuu Celestino Migliore Balozi wa Vatican
nchini Poland, wakati alipokuwa anachangia hivi karibuni katika mkutano wa mabadiliko
ya tabianchi uliokuwa umeandaliwa na Umoja wa Mataifa, mkutano ambao umehitimishwa
pasi na mafanikio makubwa, baada ya nchi wanachama kushindwa kuafikiana jinsi ya kugharimia
udhibiti wa mabadiliko ya tabianchi kwa kupunguza pia hewa ya ukaa angani. Askofu
mkuu Migliore anasema, kipeumbele cha kwanza hakina budi kutolewa kwa utu na heshima
ya binadamu, misingi ya maadili na utu wema, mafao ya wengi; hifadhi na msaada kwa
maskini na watu wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii bila kuwasahau vijana ambao ni
waathirika wakubwa wa mabadiliko ya tabianchi; kuzingatia na kuenzi haki jamii na
usawa. Mambo haya yakizingatiwa na Jumuiya ya Kimataifa kunawezekano kwa Jumuiya ya
Kimataifa kufikia muafaka juu ya mikakati inayoweza kutumiwa katika kukabiliana na
mabadiliko ya tabia nchi. Jumuiya ya Kimataifa haina budi kujikita katika mchakato
wa kulinda na kutunza ukanda wa Ozone; kuangalia kiwango cha maendeleo yaliyofikiwa
na nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa, ili kwamba, nchi changa zaidi duniani ziweze
kusaidiwa ili kupambana na athari za mabadiliko ya tabianchi pamoja na kuanza kutumia
teknolojia rafiki kwa mazingira. Suluhu za kiteknolojia ni muhimu sana, lakini wakati
mwingine hazitekelezeki. Jumuiya ya Kimataifa haina budi kuwekeza katika sera ya upashanaji
habari na elimu ya mazingita mintarafu kanuni maadili, ili kulinda pia ekolojia ya
binadamu. Athari za mabadiliko ya tabianchi zina uhusiano wa karibu na kumong’onyoka
kwa misingi ya maadili, myumbo wa uchumi kimataifa na harakati za kutafuta maendeleo
endelevu. Askofu mkuu Migliore anasema, mambo yote haya yanahitaji kwa namna ya pekee
uwajibikaji wa pamoja miongoni mwa familia ya binadamu, kwa kutoa kipaumbele cha pekee
kwa maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii.