2013-12-04 08:20:40

Liturujia inalisha na kuboresha imani; inasafisha na kupyaisha maisha adili!


Mama Kanisa anaadhimisha Jubilee ya Miaka 50 tangu Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa vatican walipochapisha hati kuhusu Mabadiliko ya Liturujia ya Kanisa inayojulikana kama “Sacrosanctum Concilium” iliyoleta mabadiliko makubwa katika Maadhimisho ya Liturujia ya Kanisa. RealAudioMP3

Nchini Italia, Maadhimisho haya yanakwenda sanjari na kumbu kumbu ya Miaka 40 tangu Baraza la Maaskofu Katoliki Italia lilipoanzisha Ofisi ya Liturujia Kitaifa kama nyenzo muhimu ya kuendeleza mabadiliko yaliyofanywa na Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican hata kwa watu wa kizazi hiki. Huu ni mchango endelevu wa Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican, changamoto kwa Taifa la Mungu kuyapokea na kuyamwilisha katika uhalisia wa maadhimisho ya Liturujia kwa nyakati hizi.

Ni mchango uliotolewa na Askofu Mariano Crociata, Katibu mkuu wa Baraza la Maaskofu Katoliki Italia, CEI ambaye ameteuliwa na Baba Mtakatifu Francisko kuwa Askofu wa Latina Terracina- Sezze Priverno, Italia, wakati alipokuwa anashiriki katika Maadhimisho ya Jubilee ya Miaka 50 ya Hati za Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican kuhusiana na mabadiliko ya Kiliturujia na Miaka 40 tangu Baraza la Maaskofu Katoliki Italia lilipoanzisha Ofisi ya Liturujia Kitaifa.

Anasema, Kanisa halina budi kuendelea kuwa aminifu kwa kumwilisha katika vipaumbele vyake Nyaraka za Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican katika maisha na utume wake, kwa kutambua kwamba, mabadiliko ya Kiliturujia imekuwa ni changamoto ya kusoma tena Injili katika uhalisia wa maisha na historia ya Kanisa; kwa kukazia ushiriki mkamilifu wa Familia nzima ya Mungu katika Maadhimisho ya Kiliturujia pamoja na kutumia lugha inayoeleweka kwa watu mahalia.

Askofu Crociata anasema, licha ya mabadiliko makubwa yaliyofanywa na Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican katika Liturujia, lakini kuna mambo mengi ambayo hayana budi kufanyiwa kazi, ili kweli lengo la Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican liweze kufikiwa. Bado Mama Kanisa hana budi kukazia malezi na majiundo ya Makleri na Waamini walei katika maisha ya Kiliturujia ili kutambua: maana na umuhimu wa Liturujia katika maisha na utume wa Kanisa; sanjari na Jumuiya ya Waamini kutolea ushuhuda wa Imani yao kwa Mungu kwa kumpatia kipaumbele cha kwanza katika maisha yao!

Ikumbukwe kwamba, kwa njia ya Liturujia ya Kanisa, Mwenyezi Mungu anawafunda watoto wake na kuwaongoza katika kulifahamu Fumbo la Ukombozi, wanapojitahidi kukutana na Kristo katika Maadhimisho ya Mafumbo ya Kanisa. Liturujia inayoadhimishwa kwa ufasaha ni jibu makini ya duku duku na maswali ya kiimani yanayoendelea kumtatiza mwanadamu wa leo.

Liturujia anasema Askofu Crociata inahitaji Katekesi ya kina na endelevu katika maisha adili ya mwamini. Wakristo wanapaswa kujenga moyo na utamaduni wa kuadhimisha imani inayojitambulisha kwa ubora wa maisha na dhamana ya waamini katika uhalisia wa maisha yao. Liturujia inalisha na kuboresha imani, inasafisha na kupyaisha maisha adili yanayojidhihirisha katika ushuhuda wa imani tendaji!









All the contents on this site are copyrighted ©.