2013-12-04 14:46:16

Kwa njia ya ubatizo, waamini wanashiriki: mateso, kifo na ufufuko wa Kristo!


Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Katekesi yake, kama sehemu ya mwendelezo wa tafakari ya kina kuhusu Kanuni ya Imani, siku ya Jumatano, tarehe 4 Desemba 2013 amegusia sehemu ya mwisho ya Kanuni ya Imani isemayo "Nangojea na ufufuko wa wafu na uzima wa milele ijayo".

Anakiri kwamba, si rahisi kuweza kuifahamu sehemu hii ya Kanuni ya Imani, lakini Injili inaonesha kwamba, ufufuko wa wafu una uhusiano wa pekee na Ufufuko wa Yesu Kristo, kielelezo kwamba kuna Ufufuko wa wafu. Baba Mtakatifu amefafanua sehemu hii ya Kanuni ya Imani kwa kukazia mambo makuu matatu yanayoonesha uhusiano uliopo kati ya ufufuko wa Kristo na ufufuko wa watu.

Maandiko Matakatifu yanaonesha hija ya imani kuelekea kwenye ufufuko wa wafu. Ni imani inaomwonesha Mwenyezi Mungu, aliyemuumba mwanadamu: mwili na roho. Huyu ni Mungu ambaye ni Mkombozi anayewajalia waja wake Roho Mtakatifu ili aweze kuwaimarisha. Ufufuko wa wafu ni mwanzo wa maisha mapya ya Waisraeli, walioshindwa vitani na kunyanyasika sana! Yesu katika Agano Jipya anaonesha ukamilifu wa Imani juu ya Ufufuko wa wafu kwa kuihusisha na maisha yake binafsi, anaposema kwamba, Yeye ndiye Ufufuko na Uzima. Siku ya mwisho, Yesu atawafufua wote wanao mwamini.

Baba Mtakatifu anasema, Yesu alifanyika mwili katika mambo yote akawa sawa na binadamu, isipokuwa hakutenda dhambi, kwa njia hii amewaachia wafuasi wake njia inayowaelekeza mbinguni kwa Baba yake. Ni Neno wa Mungu aliyefanyika mwili, aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa ajili ya binadamu; ndiye anayewakirimia wafuasi wake Roho Mtakatifu anayekamilisha umoja na Ufalme wa utukufu na uzima wa milele, ambao waamini wanausubiri kwa hamu.

Haya ndiyo matumaini yanayomwelekeza mwamini pamoja na Jumuiya ya waamini mwanga wa matumaini yanayookoa kama anavyosema Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto XVI. Wakristo ni wafuasi wa yule aliyekuja, anayekuja na atakayekuja nyakati za mwisho, mwaliko wa kutembea katika huruma na kwenye njia ya wokovu.

Baba Mtakatifu Francisko anasema, ufufuko wa wafu utakuja siku ya mwisho na kwamba, hii ni kazi inayoonesha nguvu ya Mungu atakayeifufua miili kwa kuipatia tena roho kwa nguvu ya ufufuko wa Kristo; mageuzi ambayo yanapaswa kufanyiwa kazi na waamini wakati wanapoishi hapa duniani kwa kukutana na Yesu Mfufuka katika Sakramenti, na hasa Sakramenti ya Ekaristi Takatifu. Waamini katika hija ya maisha yao hawa ndio wale wanaokula Mwili na kunywa Damu Azizi ya Yesu, ili hatimaye, kupata maisha ya uzima wa milele. Miili hii itapata utukufu na maisha ya uzima wa milele

Baba Mtakatifu anawaambia waamini kwamba, katika maisha yao hapa duniani wanashiriki pia katika Ufufuko wa Kristo, kwa njia ya Sakramenti ya Ubatizo, inayowashirikisha katika kifo na ufufuko wake ili kuwashirikisha maisha mapya, yaani ya watu waliofufuka katika Kristo. Kila mtu anashiriki katika umilele, hivyo anapaswa kuheshimiwa, kupendwa na kuthaminiwa hata katika hali ya magonjwa, ili waweze kuonja uwepo wa karibu wa Ufalme wa Mungu, ambao tayari wameanza safari ya kuuendea.

Akizungumza na mahujaji kwa lugha mbali mbali amewataka mahujaji wanaozungumza Kifaransa kukazia majiundo ya kimissionari kama njia ya kuimarisha imani katika ufufuko wa wafu! Yesu ni Hema la Mungu, linalopata makazi yake kati ya watu! Mwaliko kwa waamini kumwendea ili waweze kupata maisha ya uzima wa milele.

Kipindi cha Majilio ni wakati muafaka wa kutafakari Fumbo la Umwilisho, kielelezo cha upendo na huruma ya Mungu anayekuja kumkomboa mwanadamu. Waamini wanaalika kukesha kwa njia ya Sala, Tafakari ya Neno la Mungu pamoja na matendo ya huruma. Bikira Maria ni mfano bora wa kuigwa katika hija ya kukutana na Yesu anayekuja kati ya watu wake. Kila mwamini anakumbushwa wajibu wake wa kutangaza Injili kwa njia ya ushuhuda wa maisha, kama alivyofanya Mtakatifu Francisko Xsaveri.

Mwishoni mwa Katekesi yake, Baba Mtakatifu Francisko amewaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema kusali kwa ajili ya kuwaombea watawa waliotekwa nyara kutoka katika Monasteri ya Waothordox wa Kigriki ya Mtakatifu Tecla huko Ma'Lula nchini Syria, siku chache zilizopita. Baba Mtakatifu amewaombea watawa na watu wote ambao wametekwa nyara kutokana na vita inayoendelea nchini Syria. Kwa pamoja waendelee kusali na kusimama kidete kulinda na kutetea amani.







All the contents on this site are copyrighted ©.