2013-12-04 08:49:59

Kijiji cha Matumaini kinawekeza katika elimu ili kuwajengea wanafunzi uwezo na matumaini ya leo na kesho iliyo bora zaidi!


Padre Vincent Bosseli, muasisi wa Kijiji cha Matumaini kilichoko Jimbo Katoliki Dodoma katika mahojiano na Radio Vatican anasema kwamba, waliamua kuwekeza kwenye sekta ya elimu kuanzia: elimu ya wali ili kuwapatia watoto matumaini ya leo na kesho iliyo bora zaidi. RealAudioMP3

Ni matumaini ambayo yameibuka baada ya Kijiji cha Matumaini kuanza kutoa dawa za kurefusha maisha kwa watoto waliokuwa wameathirika kwa ugonjwa wa Ukimwi, hali iliyopelekea kuboreka na kuimarika kwa afya za watoto.

Kijiji cha Matumaini kikaaza mchakato wa ujenzi wa shule ya awali na msingi ili kuwapatia watoto fursa ya kujiendeleza kimasomo wakati huo huo wakiendelea kupata tiba ya kurefusha maisha. Ilikuwa ni vigumu kuwapeleka watoto wa Kijiji cha Matumaini kwenye shule za kawaida kutokana na ukweli kwamba: wangeweza kutengwa kutokana na unyanyapaa; idadi ya watoto ilikuwa inaongezeka kwa kasi na kwamba, watoto hawa walikuwa wanahitaji kupata tiba kwa wakati muafaka.

Ujenzi wa shule ya msingi, sekondari pamoja na kidato cha tano na sita ni mkakati wa kutaka kuvunja upweke miongoni mwa Watoto wa Kijiji cha Matumaini kwa kuwashirikisha wanafunzi kutoka katika maeneo ya jirani kusoma na kuishi pamoja na watoto walioathirika kwa Ukimwi. Shule ya Sekondari ya Kijiji cha Matumaini inaonesha mafanikio makubwa katika elimu. Padre Vincent anasema hizi ni juhudi za waalimu kutaka kuwajengea wanafunzi wao uwezo wa kiakili, ili baadaye waweze kujitegemea na kuwategemeza ndugu zao.

Ni matumaini makubwa ya Kijiji cha Matumaini kinachoendeshwa na Shirika la Masista Waabuduo Damu Takatifu ya Yesu kwamba, watoto wa Kijiji cha Matumaini wanaoendelea kukua kwa kimo na busara, siku moja watafanikiwa kuhitimu masomo yao katika medani mbali mbali za maisha na kurudi kuwasaidia watoto wengine wanaoendelea kupambana na ugonjwa wa Ukimwi ndani na nje ya Kijiji cha Matumaini, kama sehemu ya mchakato wa kutangaza Injili ya Furaha na Matumaini kwa wale waliokata tamaa kutokana na ugonjwa wa Ukimwi.







All the contents on this site are copyrighted ©.